Zitto Kabwe kukata rufaa dhidi ya hukumu


0
Zitto Kabwe mahakamani leo, 29 Mei 2020

 

Dar es Salaam, Tanzania

Mahakama ya Kisutu nchini imemtia hatiani kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kwa makosa ya uchochezi lakini imemwachia huru kwa sharti la kutotoa au kutoandika kauli za kichochezi katika kipindi cha mwaka mmoja.
Zitto Kabwe alifikishwa kwa mara kwanza mahakamani Novemba 2, mwaka 2018 kwa makosa ya kutoa kauli hizo za uchochezi kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika October 28, 2018.
Mashtaka ya Zitto yanatokana na kauli zake za kulitaka jeshi la polisi kutolea maelezo ya kile alichokiita mauaji ya polisi dhidi ya raia yaliyotokea kwenye Kijiji cha Mpeta wilayani  Uvinza, mkoani Kigoma. Katika kesi ya msingi Zitto alisomewa mashtaka matatu ya uchochezi ikiwemo kutoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki, kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya jeshi la polisi
Februari 18 mwaka huu Zitto alikutwa na kesi ya kujibu na hivyo kuanza kujitetea kwa siku nne mfululizo kutoka Machi 17 hadi 20.Baada ya kesi kuunguruma kwa zaidi ya mwaka mmoja, leo Mahakama hiyo imemtia hatiani Zitto kwa makosa yote matatu ya uchochezi yaliyokuwa yanamkabili.

Makamu mwenyekiti wa Chama cha ACT, Dorothy Semu, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema kuwa hukumu dhidi ya kiongozi wao haikubaliki na wataipinga mahakamani kwani ni sawa na kumzuia Zitto kusema chochote cha kuikosoa serikali na rais katika mwaka wa uchaguzi.

Amebainisha kuwa Kiongozi wao Zitto Kabwe yupo imara na hukumu hiyo haitomrudisha nyuma. Waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia katika mahakama hiyo wakati hukumu ikitolewa.


Like it? Share with your friends!

0