WHO:Mtu mmoja kati 25 ana magonjwa ya zinaa


0

Kiwango cha kimataifa cha maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STI), kinapaswa kuwa kengele ya kuziamasha Serikali, kutokana na kwamba magojnwa hayo yameoonekana kuongezeka katika mataifa mengi ulimwenguni.

Kwa mujibu wa wataalam wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya afya, takwimu zinazoonyesha kwamba mtu mmoja kati ya 25 ana maradhi ya zinaa yanayotibika ambayo hutokea katika kiwango cha maambukizi zaidi ya milioni moja kwa siku.

Wataalam hao wameonyesha  wasiwasi wao hasa katika kukosekana hatua madhubuti za nchi kukomesha kusambaa kwa maambukizi ya magonjwa hayo na mengine ya zinaa.

Shirika la afya ulimwenguni WHO, limeonya kwamba endapo maradhi hayo yataachwa bila kutibiwa  yanaweza kuwa na athari kubwa katika afya hasa ya vijana, watu wazima na watoto ambao bado hawajazaliwa.

Akisistiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka zaidi Dkt. Peter Salama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa huduma ya afya kwa wote wa WHO amesema “Hii ni kengele ya kuziamsha pande zote husika katika kuchukua hatua za pamoja ili kuhakikisha kila mtu , kila mahali anaweza kupata huduma anazohitaji katika kuzuia na kutibu magonjwa haya za zinaa”

Kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya wataalam hao athari mbaya za magonjwa manne mashuhuri ya zinaa yanayotibika ambayo ni klamidia, kisonono, kaswende na muwasho sehemu za siri ni pamoja na athari za mishipa, kutozaa, kupoteza ujauzito, matatizo wakati wa ujauzito, watoto kufia tumboni na ongezeko la hatari ya kuambukizwa HIV.

Dkt. Melanie Taylor mtaalam wa masuala ya kisaikolojia wa WHO katika idara ya afya ya uzazi na utafiti  anasema “Kwa wastani takwimu hizo zinaonyesha kuwa nmtu mmoja kati ya 25 duniani kote angalau ana aina moja ya magonjwa ya zinaa yanayotibika huku wengine wakiambukizwa zaidi ugonjwa mmoja kwa wakati mmoja, na hivyo kuibebesha dunia mzigo mkubwa wa STI, WHO mara ya mwisho ilichapisha takwimu za magonjwa ya zinaa mwaka 2012 na hadi sasa maambukizi ya magonjwa hayo hayajapungua sana.”

Matokeo ya utafiti wa kimataifa wa  WHO kwa mwaka 2016 yameonyesha kwamba kwa wanawake na wanaume wa umri wa miaka kati ya 15-49, kuna maambukizi zaidi ya milioni 376, huku magonjwa ya muwasho yakiongoza kwa visa milioni 156, ukifuatiwa na klamidia visa milioni 127, huku kisosnono kikiwa na visa milioni 87 na kaswende visa milioni 6.3. Kwa ujumla magonjwa haya kwa mwaka 2016 yamesababisha watoto takribani 200,000 kufia tumboni na pia idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga na kufanya kuwa sababu iliyoongoza kwa vifo vya Watoto duniani kwa mwaka huo.

Ingawa WHO inasema magonjwa haya yanaweza kutibika na aina mbalimbali ya dawa  zilizopo , limeonya kwamba upungufu mkubwa duniani kote wa hivi karibuni wa dawa aina za benzathine penicillin, umefanya kuwa changamoto kutibu ugonjwa wa kaswende. Pia ripoti inasema usugu wa viuasumu kwa dhidi ya ugonjwa wa kisonono nao umekuwa ni moja ya tishio la kiafya linaloongezeka na huenda ukasababisha kuwa vigumu kutibu ugonjwa huo

Kwa ujumla bakteria zaidi ya aina 30, virusi na wadudu wengine wanajulikana kwa kuambukizwa kupitia ngono isiyosalama. Lakini via maradhi mengine yanaweza kuambukizwa kwa kupewa damu iliyoambukizwa pamoja na kutumia sindano zisizosalama hasa miongoni mwa watumiaji wa mihadarati.

Mbali ya magonjwa haya manne yaliyotajwa kwenye ripoti ambayo yanatibika aina zingine nne ni za virusi visivyotibika ambazo ni homa ya ini aina B, virusi vya malenglenge aina 1 na 2 au HSV, virusi vya HIV na HPV.

Pia shirika hilo linasema magonjwa mengi ya zinaa yanaweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto  wakati wa ujauzito au kujifungua ikiwemo klamidia, kisosnono, homa ya aini aina B, HIV na kaswende.

Kwa mantiki hiyo WHO, inasema upimaji kwa wakati na matibabu ni muhimu sana katika kupunguza mzigo wa magonjwa hayo ya zinaa kimataifa na shirika hilo limetoa wito kwa kina mama wajawazito kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara hasa kwa maradhi ya kaswende na HIV.


Like it? Share with your friends!

0