WHO yahimiza utokomezaji wa Homa ya Ini.


0

Kuelekea siku ya kutokomeza homa ya ini Julai 28, Shirika la Afya ulimwenguni, WHO limetoa wito kwa nchi kuchukua fursa kufuatia kupungua kwa gharama ya kuchunguza na kutibu Homa ya Ini, inayoambukiza na kuimarisha uwekezaji katika kutokomeza ugonjwa huo kabisa.

Taarifa ya WHO iliyochapishwa leo, kutokana na utafiti wa shirika hilo inasema kwamba, kwa kuwekeza dola bilioni 6 kwa mwaka inawezekana kutokomeza Homa ya Ini katika nchi 67 za kipato cha chini na cha wastani, na kuzuia vifo milioni 4.5 kufikia mwaka 2030 na zaidi ya vifo milioni 26 katika siku zijazo.

WHO inasema pia dola bilioni 58.7 zinahitajika katika kutokomeza Homa ya Ini inayoambukiza kama tishio la afya ya umma katika nchi 67 kufikia mwaka 2030. Hii inamaanisha kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo kwa asilimia 90 na kupunguza vifo kwa asilimia 65. Moja ya njia ya kupunguza maambukizi ni chanjo kama anavyofafanua Dkt. Marc Butlery kutoka kitengo cha Homa ya Ini kwenye shirika la WHO.

(Sauti ya Dkt. Butlery)

“Kitu muhimu katika kuzuia ugonjwa ni kutoa chanjo hususan kwa watoto kwa sababu kuna maambukizi mengi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambapo asilimia 90 ya maambukizi ya homa ya ini aina B hutokea mapema maishani kwa hiyo ni muhimu kwa nchi kuanzisha chanjo hii pindi tu mtoto anapozaliwa na WHO inatoa msukumo kwa nchi zote kutekeleza hilo iki maanisha kwamba mtoto anapewa chanjo ya homa ya ini ndani ya saa 24 anapozaliwa na dozi zingine mbili hadi tatu wakati akiwa bado mchanga.”

Kwa mujibu wa Dkt. Marc Butlery kutoka kitengo cha Homa ya Ini kwenye Shirika la WHO, amesema kwamba ili kuzuia Homa ya Ini aina C, WHO inasisitiza sindano zinazotumika katika vituo vya afya au hata kwingineko lazima ziwe mpya na ziwe salama.

Halikadhalika Dkt. Butlery ametolea mfano Misri ambayo ni miongoni mwa nchi zilizotajwa kuwa na mzigo mkubwa wa homa ya ini akisema

“Kwa hiyo wameimarisha program zao na sasa wanafanya uchunguzi kwa ajili ya Homa ya Ini aina B na C, lakini pia wanatoa matibabu ya bure kwa jamii na kwa sasa wamepunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa na sasa Misri itasaidia nchi nyingine kupunguza mzigo wa homa ya ini aina C.


Like it? Share with your friends!

0