Wawekezaji watakiwa kufuata sheria nchini


0

Serikali imewataka wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini kufuata sheria na taratibu za nchi ili kuepuka matatizo katika ulipaji kodi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, alitoa tahadhari hiyo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma alipotembelea mgodi mpya wa uchimbaji makaa ya mawe wa Mil coal.

Alisema baadhi ya wawekezaji wanatumia njia za mkato na kukwepa kulipa kodi, hali inayosababisha kuingia kwenye migogoro isiyokuwa na tija.

Waziri Kairuki alisema Serikali haipendi kuona matatizo katika uwekezaji wowote nchini kwa kuwa lengo ni kuhakikisha uwekezaji unaleta tija kwa taifa na kwa jamii inayowazunguka.

“Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo mbalimbali na haitapenda kuona mwekezaji yeyote wa ndani na nje ya nchi, anashindwa kuwekeza kwa sababu yoyote ile ambayo siyo ya msingi,” alisema.

Pia, aliwataka wawekezaji kutoa taarifa kwa ngazi nyingine endapo wataona kuna mahali wanakwama au kukwamishwa na mtumishi yeyote wa Serikali au taasisi na kuitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizopo nchini kuwekeza na pale wanapoona uwezo wao ni mdogo ni vyema wakatafuta wageni wenye uwezo wakashirikiana nao.

Alisema Serikali itaendelea kusimamia stahiki za wawekezaji wazawa ambao wanashirikiana na wawekezaji kutoka nje kuhakikisha wanapata asilimia zao za uwekezaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Kwa upande wao wawekezaji wa mgodi huo, Mussa Charles na Vidya Sagar, wameeleza mipango ambayo tayari wameanza kutekeleza hasa upande wa kutoa huduma za jamii ikiwamo ujenzi wa barabara.

Wameelezea pia mipango yao ya baadaye watakapoanza kuzalisha kwa kuwa kwa sasa wana muda wa wiki tatu pekee na wameanza kazi ya kutengeneza barabara na wataendelea kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wanaowazunguka.

Waziri Kairuki alitoa mfano wa mgodi wa kuchimba makaa ya mawe wa Ngaka Tancoal ambao unadaiwa na Serikali kodi ya zaidi ya shilingi bilioni 23, licha ya Serikali kutoa maelekezo muda mrefu kuhusu kupeleka utaratibu watakavyoanza kulipa deni hilo, lakini hadi sasa wameshindwa.


Like it? Share with your friends!

0