Watoto milioni 108 hutumikishwa duniani


0

Ikiwa leo ni siku ya kupinga ajira kwa watoto ambayo kila mwaka dunia huadhimisha siku hiyo ifikapo tarehe 12 Juni, Shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO limesema bado watoto wanaendelea kutumikishwa kwenye sekta ya kilimo ulimwenguni kote, na hivyo kuathiri uwezo wao wa kustawi na kujinasua kwenye umaskini pindi wanapokuwa watu wazima.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka FAO zinasema duniani kote watoto milioni 108 wa kike na wa kiume, wanatumikishwa ambapo asilimia 70 wanafanya kazi kwenye sekta za kilimo, ufugaji, misitu, uvuvi na ufugaji wa samaki.

Idadi hiyo, kwa mujibu wa FAO imeongezeka kwa watoto milioni 10 tangu mwaka 2012, licha ya jitihada za Umoja wa Mataifa za kutokomeza utumikishaji watoto kwenye sekta hizo.

Ariane Genthon ambaye anahusiska na miradi ya FAO ya kuondokana na utumikishwaji wa watoto kwenye kilimo, anasema sababu kubwa ni umaskini kwenye familia ambao husababisha wazazi kutumia watoto wao kufanya kazi kwenye kilimo.

Amesema watoto wanapotumikishwa kwenye kilimo wanashindwa kwenda shule, na hata pale wanapokwenda wanakuwa wamechoka na wanashindwa kusoma ipasavyo kama wenzao ambao hawaendi kwenye kilimo.

Bi. Genthon amesema pamoja na uchovu, watoto wanakuwa wanakumbwa na madhara ya kiafya kutokana na kemikali zinazotumika kwenye sekta ya kilimo na mara nyingi wazazi hutumia watoto wao kwa kuwa wanafanya kazi bila ujira.


Like it? Share with your friends!

0