Watoto 6,376 nchini wafanyiwa ukatili wa kingono


0

Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), imeeleza kuongezeka kwa ukatili dhidi ya Watoto kwa kiasi kikubwa hususani ukatili wa kingono hasa ubakaji na ulawiti

Ripoti hiyo ya mwaka 2018 ambayo imezinduliwa leo imetaja kuongezeka kwa matukio hayo kutoka 4728 kwa mwaka 2017 hadi kufikia 6,376 katika kipindi cha mwaka 2018, ambapo pia uhuru dhidi  ya ukatili imeonekana kukiukwa zaidi Tanzania Bara, na sababu kubwa inatajwa jamii yenyewe.

Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Anna Henga, anasema jambo hilo halipaswi kufumbiwa macho ni wakati wa jamii, wazazi, walezi, wanaazaki, viongozi wa dini na serikali kwa ujumla kutafuta namna ya kulikomesha, kwani vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto vinavyoendelea hapa nchini vinakiuka mikataba ya kimataifa ukiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za mtoto ulioidhinishwa mwaka 1989, na ule Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1990.

Ripoti hiyo ilikwenda kwa jina la Ukatili wa Kingono, Tishio kwa Haki na Ustawi wa Mtoto nchini Tanzania, imeweza pia kuangazia haki za wanawake, haki za makundi maalum, haki za maendeleo, ubaguzi dhidi ya Watoto, uhuru wa kukusanyika, haki za kiraia na nyinginezo, ambapo miongoni mwa matokeo chanya katika ripoti hiyo ni kupungua kwa hukumu za vifo, kwani katika ripoti hiyo,  kwa mwaka 2018 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), kilikusanya matukio matano ya hukumu ya kifo, ukilinganisha na mwaka 2017 iliyokuwa na matukio 15.

Mtafiti katika ripoti hiyo bwana Fundikila Wazumbi anasema jambo hilo kwa Serikali ni hatua nzuri, ikizingatiwa kuwa hata Rais mwenyewe alikataa kupelekewa hukumu za vifo, ingawa maboresho ya sheria hiyo yanahitajika kwa kua haina funzo, na hata nchi zinazotekeleza hukumu hiyo hadi sasa bado hazijaweza kudhibiti wahalifu.

Ripoti hiyo pia imeweka wazi kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wanawake ambapo mikoa ya kanda ya Kaskazini inaongoza kwa ukatili wa ubakaji ambapo wanawake wamekuwa wakifanyiwa na waume zao, ikiwamo kuingiliwa kinyume na maumbile.

Ripoti ya LHRC imehusisha Tanzania Bara na Zanzibar, lakini imetaja mikoa isiyopungua 9 kuangaliwa zaidi, katika masuala ya haki za binadamu ambayo ni Mwanza, Tabora, Dar es salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Shinyanga, Singida na Kigoma. 

 

 


Like it? Share with your friends!

0