Watakaosafirisha mifuko ya plastiki kutozwa faini milioni 20


0

Tarehe 1/6/2019, ndio siku rasmi ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki inaanza kufanya kazi, licha ya wengi kuwa na maswali juu ya utekelezwaji wa marufuku hiyo.

Nikualike katika Makala haya, kuangazia  masuala ya mifuko ya plastiki, na katazo lililotolewa na Serikali siku za hivi karibuni.

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 9 Aprili, 2019, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, akiwa bungeni alitangaza kupiga marufuku uingizwaji na uzalishaji wa mifuko ya palstiki, huku lengo likiwa ni katika kutunza mazingira kutokana na kwamba bidhaa hiyo imetajwa kuwa mwaribifu mkubwa wa mazingira.

Nikukumbushe tuu, mifuko ya plastiki ilianza rasmi mnamo mwaka 1970, lakini licha ya kuwa inaingizia mataifa mengi pesa nyingi, wataalam wa afya wanadai kuna athari kubwa za kiafya zitokanazo na matumizi ya mifuko hiyo ikiwamo magonjwa ya Saratani.

Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira zinaeleza kuwa duniani kote mifuko trilioni 5 huzalishwa, ambayo ni sawa matumizi ya mifuko miwili kwa kila mtu mmoja kwa siku.

Takribani 60% hadi  80% ya mifuko huwa inatupwa hovyo kila siku, hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira.

Nchini Tanzania hususani Tanzania Bara, kila mtanzania mmoja anatumia mfuko 1 hadi 2 kwa wiki, ambapo kwa mwaka matumizi huwa bilioni 3.

Unaposema Tanzania Bara ndio kuna matumizi makubwa ya mifuko ya plastiki unaweza ukajiuliza ni kwanini hasaa Tanzania Bara na si Visiwani (Zanzibar)?.

Jibu ni kwamba katika mafanikio ya kuzuia matumizi ya mifuko ya Plastiki Zanzibar, imefanikiwa katika zoezi hilo huku Tanzania Bara ikiwa bado haijafanikiwa licha ya kuwa na mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo kwa zaidi ya miaka 15 sasa.

Wakati Zanzibar ikiwa imefanikiwa huku Bara 80% ya mifuko huzalishwa na 20% inaingizwa kutoka nje ya nchi, na 84% ya mifuko hiyo huishia kwenye mazingira ya watu.

Mifuko ya Plastiki hudumu kwa muda wa miaka 500 hadi 1000, jambo ambalo linatajwa kuleta atahari kubwa ya kimazingira na hata kwa viumbe hai.

Miongoni mwa maeneo yanayoathiriwa na mifuko ya plastiki ni katika hifadhi za wanayama, ambapo inaelezwa kuwa takwimu za mwaka 2017/2018, kulikuwa na vifo 153 vya ng’ombe na kati ya hivyo vifo 56, vimetokana na kula mifuko.

Hata hivyo Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira limeendelea kuonya kuwa ifikapo 2050, takataka za plastiki zitakuwa nyingi kuliko samaki, ambapo inakadiriwa kila mwaka viumbe hai wa baharini wapatao 100,000 hufa.

MAADHIMIO YA BARAZA LA UMOJA WA MATAIFA LA MAZINGIRA.

Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira, mwaka 2014 liliazimia kuwa uchafuzi unaotokana na Plastiki ni changamoto ya kidunia. Zaidi ya nchi 127 duniani zimechukua hatua katika kukabiliana na Plastiki.

Hatua zilizochukuliwa na nchi hizo katika kukabiliana na changamoto ya mifuko ya Plastiki, ni pamoja na.

  1. Kupiga marufuku uzalishaji wa mifuko hiyo.
  2. Kuongeza kodi.
  3. Kuruhusu mifuko yenye unene maalum.

Hadi sasa nchi 25, zimeweza kupiga hatua katika udhibiti wa mifuko ya Plastiki, lakini Tanzania imejaribu kuchukua hatua lakini imeshindikana na miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara, ilisitisha usajili mpya wa viwanda vya uzalishaji mifuko mwaka 2006.

Hata hivyo kwa sasa, Serikali, imeweka bayana kanuni na sheria, ambazo zimechambua adhabu za atakayekutwa na mifuko.Katika kanuni hizo zimesamehe vifungashio vya viwandani, vifungashio vya chakula na n.k.

Wakati huohuo sheria imetaja kumtoza faini ya shilingi 30000, mtu atakayekutwa na mifuko hiyo, huku yule atakayeonekana kusafirisha bidhaa hiyo atapigwa faini ya shilingi milioni 20, au kifungo cha miezi 6 jela, ama vyote kwa pamoja.

Waziri mwenye dhamana ya Mazingira Januari Makamba, anasema ili zoezi hilo lifanikiwe ni lazima jamii ipewe elimu ya kutosha kuhusu madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki, huku akionya mamlaka za ngazi ya chini, ukianzia Serikali ya Mtaa, kuacha kutumia nguvu katika zoezi la kusaka mifuko hiyo.

“Tutapita kwenye maduka na magenge kuona kama bado kuna matumizi ya mifuko ya plastiki, hatutegemei kusimamisha watu njiani na kuanza kuwafanyia upekuzi kwenye mifuko na mabegi yao kuona kama wanahifadhi mifuko ya plastiki” – Waziri wa Mazingira, January Makamba.

Kadhalika Waziri Makamba anaonya utozaji wa faini isiwe chanzo cha mapato, kwani mabadiliko ni jambo gumu sana, kwani jamii ilishazoea hivyo kuibadilisha inahitaji muda.

Suala lililobaki hivi sasa katika marufuku hii ni utekelezaji, je utekelezaji huo utazingatiwa?.

 

 

 


Like it? Share with your friends!

0