Washtakiwa wa uhujumu uchumi wajitokeza kuomba msamaha


0

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Balozi Augustine Mahiga amesema washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi walio tayari kuomba msamaha na kusamehewa wameanza kufanya hivyo kwa kasi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Mahiga ametoa kauli hiyo katika mahojiano na televisheni ya Azam jana Jumanne Septemba 24, 2019.

Amesema DPP, Biswalo Mganga ameanza kupokea maombi hayo kwa kasi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa pendekezo la Rais wa Tanzania, John Magufuli alilolitoa juzi baada ya kumaliza kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Magufuli alitoa siku saba kwa washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi walio tayari kuomba msamaha kufanya hivyo, huku akiweka sharti kwamba wanaostahili msamaha ni wale watakaokuwa tayari kurudisha fedha walizotakatisha.

“Hapa tunavyozungumza nimetoka kuzungumza na DPP ananiambia maombi yanaingia kwa kasi sana na sasa lazima wafanye uchambuzi.”

“Si suala tu la kutazama kesi moja, lazima kutazama mafaili, kutazama chimbuko lake kwa kushirikiana na idara ya upelelezi,” amesema Balozi Mahiga,.

Mganga ambaye pia alihojiwa na televisheni hiyo amesita kuitaja idadi ya watuhumiwa wanaohusika na kusisitiza kuwa idadi yao hatoitaja.

“Akiamua kukaa kule (mahabusu) tutaendelea naye  akisema jamani mimi niko tayari kuomba msamaha tutaongea ila kwa hiyo minong’onong’o tuyaache tu.”

“Mshtakiwa mwenyewe au kwa kupitia mawakili wake akiwa mahabusu ataandika barua mwenyewe ili kesho na kesho kutwa asije kuiruka Serikali ndio maana watuhumiwa wenyewe wanaandika,” amesema Mganga.


Like it? Share with your friends!

0