Wakurugenzi wapigwa marufuku kusimamia uchaguzi


0

Mahakama Kuu imefuta sheria iliyokuwa inawapa wakurugenzi wa halmashauri mamlaka ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi, uamuzi ambao utalazimisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuteua watu wake badala ya kutegemea wateule hao wa Rais, iwapo hautabadilishwa na Mahakama ya juu.

Mahakama Kuu pia haijaiamuru Serikali kubadilisha vifungu vilivyoonekana vinakwenda kinyume na Katiba baada ya watetezi, wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya siasa kufungua kesi hiyo wakitaka vitamkwe kuwa batili.

Jaji Atuganile Ngala, ambaye alisaidiana na majaji Benhajj Masoud na Firmin Matogolo, alitoa uamuzi huo jana katika kesi hiyo ya kikatiba iliyofunguliwa mwaka 2018

Katika kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe, aliyekuwa mdai pekee, alikuwa anapinga wakurugenzi hao wa halmashauri za wilaya, manispaa na au majiji kuwa wasimamizi akidai kuwa ni kinyume cha Katiba.

Katika uamuzi wake jana, Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za Wangwe dhidi ya utetezi wa Serikali iliyojitetea kuwa suala hilo haliathiri uchaguzi kwa kuwa uteuzi wao ni kwa mujibu wa sheria.

Jaji Ngwala alisema vifungu 7(1), kinachowapa wakurugenzi mamlaka ya kusimamia uchaguzi, na 7(3) vya Sheria ya Uchaguzi vinakwenda kinyume na matakwa ya kikatiba ya uhuru wa Tume ya Uchaguzi.

Alisema wakurugenzi hao ni wateule wa Rais na hawako chini ya Tume, wakati Katiba inaelekeza NEC iwe chombo huru.

Jaji Ngwala pia alisema sheria hiyo haihakikishi kuwa wakurugenzi hao wanakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema wameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mdai kuwa wakurugenzi wengi ni wanachama wa CCM, baada ya Mahakama kupewa orodha ya wakurugenzi 74 wanachama wa chama hicho tawala.

Kifungu cha 7(3) kinaeleza kwamba NEC inaweza kumteua mtu yeyote kuwa msimamizi, lakini Mahakama ilisema hakiweki ulinzi kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa huru, na kwamba lazima kuwe na ulinzi kwa kuhakikisha kuwa anayeteuliwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa.

“Kwa hiyo tunatamka kwamba vifungu hivi ni kinyume cha Katiba ya nchi inayotaka kuwe na uhuru wa tume katika utekelezaji wa majukumu yake,” alisema.

Uamuzi huo ulipokewa kwa furaha na Wakili Fatma Karume aliyemwakilisha Wangwe.

“Kwa uamuzi huu, sasa hakuna wasimamizi wa uchaguzi. Itabidi NEC itumie kifungu cha 7(2) cha sheria hiyo kuteua wasimamizi huru,” alisema.

Wakili Karume alifurahishwa na kitendo cha Mahakama kutotoa amri kwa Serikali ya kufanya marekebisho ya sheria hiyo wala kuipa muda.

“Maana yake ni kwamba imevifuta moja kwa moja badala ya kuipa Serikali nafasi,” alisema.

“Kwa hiyo nimefurahi sana, sana kwa uamuzi huu kwa sababu hatukuwa na tume huru kwa kuwa wale waliokuwa na jukumu la kuhesabu na kuhakikisha kuwa kura ziko salama hawakuwa huru, kwa sababu hawakuwa chini ya Tume bali chini ya Rais na chama tawala.”

Naye Wangwe aliuenzi uamuzi huo kwa watu wote wanaopenda demokrasia na wasiopenda harakati.


Like it? Share with your friends!

0