Wahamiaji 150 wahofiwa kufa baada ya boti kuzama pwani ya Libya


0

Zaidi ya wahamiaji 100, waliokuwa wakielekea Ulaya, hawajulikani waliko na inahofiwa wamepoteza maisha baada ya boti walizokuwa wakisafiria kuzama katika bahari Mediterrania katika pwani ya Libya.

Hayo yamesemwa na shirika la Umoja wa Mataifa, linalowashughulikia wahamiaji pamoja na walinzi wa pwani nchini Libya.

Ayoub Gassim ambaye ni msemaji wa walinzi wa pwani nchini Libya, ameliambia shirika la habari la Associated Press, kuwa boti mbili zilizowabeba takriban wahamiaji 300 zilizama yapata kilomita 120 mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Ameongeza kuwa wahamiaji 137 waliokolewa na kurudishwa Libya lakini hadi sasa walinzi wa pwani wamefaulu kuopoa mwili mmoja pekee.

Charlie Yaxley ambaye ni msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, amesema wanakadiria kuwa wahamiaji 150 miongoni mwao wanawake na watoto, hawajulikani waliko na wanahofuwa kufariki.


Like it? Share with your friends!

0