Viongozi wanne wa CHADEMA wakamatwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya


0

Viongozi wanne wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), mkoani Kilimanjaro akiwemo Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Owenya, wamekamatwa na Polisi kwa amri ya Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Lucy na viongozi wengine, wamekamatwa leo Ijumaa Septemba 20, 2019, kwa tuhuma za kwenda shule ya Sekondari ya Rundugai wilayani humo na kufanya siasa kinyume cha utaratibu.

Wengine waliokamatwa ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu, Katibu wa Mbunge wa Hai, Irene Lema na Diwani wa Machame Kaskazini, Clement Kwayu.

Sabaya amesema kuwa viongozi hao walikwenda katika shule hiyo leo Ijumaa asubuhi kwa madai ya kuzungumza na wanafunzi na kutoa misaada, bila mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwa na taarifa.

“Kuna maelekezo ya mheshimiwa Rais (John Magufuli) kuwa yeyote anayetaka kutoa misaada katika shule yeyote atoe taarifa kwa mkurugenzi wa Halmashauri ili misaada hiyo ijulikane, lengo lake na iweze kuratibiwa,” amesema Sabaya.

Sabaya amedai badala yake, viongozi hao walikwenda katika shule na wamekuwa wakifanya hivyo mara kwa mara bila kutoa taarifa, jambo linalokiuka maagizo na maelekezo ya Serikali.

Viongozi hao wamepelekwa katika kituo cha Polisi Bomang’ombe, na taratibu zingine za kisheria zinafata.

 

 

 

 

 


Like it? Share with your friends!

0