Vinara wanne wenye kiu ya urais Chadema


-2
-2 points

TANZANIA

Ni majuma mawili yamepita tangu chama kikuu cha upinzani nchini Chadema, kufungua mlango kwa wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu. Hadi sasa, wananachama wanne wameonesha nia ya kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu kupitia chama hicho.

Mchakato wa kutia nia kuwania urais ulianza Juni 3 hadi 15, mwaka huu, baada ya kipenga kupulizwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Kwanza TV inaangazia wasifu wa kila mgombea miongoni mwa hao, ikiwa leo ndio hitimisho la mchakato wa kutia nia.

Tundu Antiphas Mughwai Lissu:

Huyu anajulikana zaidi kama mwanasiasa machachari, mjuzi wa masuala ya sheria na ujasiri wa kutenda na kutamka kile anachokiamini. Kwa ufupi ni sawa na kusema, ni mtu jasiri.

Alizaliwa Januari 20, 1968 katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kusoma katika Shule ya Msingi Mahambe iliyopo Singida kuanzia mwaka 1976 hadi 1982. Kisha alijiunga na kupata elimu ya sekondari katika shule ya Galanos iliyopo mkoani Tanga kati ya mwaka 1987 hadi 1989.

Baada ya hapo, Lissu alijiunga na sekondari ya juu kwa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya wanafunzi wenye vipaji – Ilboru iliyopo mkoani Arusha. Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 1983 hadi 1986.

Lissu alichukua shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1991 hadi 1994, kisha alikwenda nchini Uingereza kuchukua shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Warwick. Hiyo ilikuwa kati ya mwaka 1995 hadi 1996.

Siasa:

Lissu alianza kujulikana zaidi katika masuala ya siasa miaka mitatu baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 1992. Hiyo ilikuwa ni mwaka 1995 alipojiunga NCCR – Mageuzi, wakati huo ikiongozwa na Augostino Mrema.

Mwaka 2010, Lissu alichaguliwa kuwa mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya Chadema na baada ya kipindi cha miaka mitano kumalizika, alirejea tena bungeni kupitia chama hicho, akiliwakilisha jimbo la Singida Mashariki.

Ilipofika mwaka jana (2019), Lissu aliingia katika historia ya kuwa mbunge wa kwanza nchini kuvuliwa wadhifa huo akiwa nje ya nchi kwa matibabu yaliyotokana na kupigwa risasi zaidi ya 20.

Ilikuwa shangwe kwa baadhi ya washindani wake wa kisiasa, lakini huzuni iliwajaa wengine walioshindwa kuzuia hisia zao na kukifananisha kitendo hicho kama kilichovuka mpaka wa utu katika uongozi wa umma.

Kwa miaka kadhaa sasa, Lissu amejijengea sifa kama wakili mashuhuri, mwanasiasa shupavu wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa serikali hasa ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Kunusurika kifo:

September 7, 2017 Lissu alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana.

Alipelekwa nchini Kenya kwa matibabu zaidi na baadaye alisafirishwa hadi Ubelgiji alipoendelea kufanyiwa upasuaji kwa takribani mara 22, ikiwa ni moja ya idadi kubwa ya upasuaji kwa binadamu.

Juni 8, mwaka huu, Lissu alitangaza rasmi nia ya kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa ahadi kadhaa ikiwemo kuzifuta sheria alizoziita kandamizi na zinazotumika kuminya uhuru hasa wa kujieleza kwa raia.

Lazaro Nyalandu

Ni mwanasiasa asiyekuwa na hulka ya kuongea sana. Ana mazoea ya kujituma kufanya kazi kama ambavyo vijana wa kisasa wanapenda kuita, “ni mtu wa hekaheka”.

Alizaliwa Augosti 1970. Alikuwa miongoni wa wanachama wa muda mrefu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alimokuwa kabla ya kujiunga Chadema.

Akiwa CCM, aliwahi kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kati ya Januari 20, 2014 hadi Novemba 5, 2015, ikiwa ni baada ya kuchaguliwa Mbunge wa Singida Kaskazini mwaka 2010.

Elimu:

Alisoma shule ya msingi ya Pohama ya mkoani Singida na baadaye alijiunga katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha mkoani Pwani, alipohotimu kidato cha nne na kuchaguliwa kujiunga katika Shule ya Sekondari ya Illboru mkoani Arusha.

Katika safari yake hiyo ya masomo kote alikopita alifanikiwa kufaulu katika daraja la kwanza kila alipofanya mitihani ya kuhitimu.

Nyalandu alisoma shahada ya kwanza ya masuala ya utawala wa kibiashara katika Chuo Kikuu cha Wartburg kilichopo nchini Marekani, na baadaye shahada ya pili katika chuo cha Buckingham nchini Uingereza.

Kabla ya kujiunga na siasa, Nyalandu alifanya kazi ya Mshauri wa masuala ya kimatiafa na maendeleo wa Equal Opportunity Trust Fund kuanzia 1999 hadi 2000, lakini pia aliwahi kufanya kazi benki katika mji wa Minneapolis nchini Marekani mwaka 1998 hadi 1999.

Siasa

Alisikika zaidi katika siasa mwaka 2000 baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM, nafasi aliyodumu nayo mpaka alipojiuzulu, kutoka katika chama hicho na kujiunga Chadema.

Urais

Juni 14, mwaka huu, Nyalandu alitangaza nia ya kuwania urais kupitia Chadema, akifuata nyayo za Lissu. Lakini yeye (Nyalandu) anaahidi kuleta maendeleo endevu kwa Taifa linalosimamia uhuru na haki za watu, utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na demokrasia ya kweli inayowapa wananchi mamlaka ya juu kwa mustakadhi na mwelekeo ya nchi kupitia chaguzi zilizo huru na za haki.

Mchungaji Peter Msigwa

Alizaliwa Juni 8 mwaka 1965. Ni mbunge wa jimbo la Iringa Mjini kuanzia mwaka 2010 mpaka sasa, akiwa Chadema.

Alisoma Shule ya Msingi Magoye iliyopo Njombe mwaka 1977 hadi 1981, na baadaye kujiunga elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Sangu kwa kipindi cha mwaka 1983 hadi 1986.

Baada kumaliza kidato cha nne, alijiendeleza katika ngazi mbalimbali nchini Afrika Kusini akianzia kiwango cha cheti, stashahada na shahada katika Chuo Kikuu cha Durban.

Alijitokeza zaidi katika siasa mwaka 2005 akiwa mwanachama wa Tanzania Labour (TLP) ikiongozwa na Mrema ambaye hadi sasa ndiye Mwenyekiti wa chama hicho.

Mwaka 2006, Mchungaji Msigwa alijiunga na Chadema, chama anachoendelea kukitumikia na sasa anaomba ridhaa ya kuteuliwa ili awanie urais.

Mwaka 2010, alichaguliwa kuwa mbunge kwa kumshinda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na mbunge wa jimbo Monica Mbega na kisha kuchaguliwa tena mwaka 2015 hadi sasa.

Dr Rosemary Kavura Majinge

Huyu ni kada nguli aliyetokea Chama Cha Mapinduzi (CCM), akishika nyadhifa mbalimbali na baadaye kutikisa katika kuwania moja ya nafasi kubwa za uongozi katika Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho (UWT).

Moja ya matukio ya kisiasa yaliyomsibu Majinge ni wakati wa kuwania kuteuliwa na CCM kuwania ubunge katika jimbo la Ukonga. Yeye na waliokuwa wagombea wenzake ‘waliburuzwa vibaya’ na aliyekuwa mbunge wa Ukonga Dk Milton Makongoro Mahanga (marehemu).

Hadi tunachapisha makala haya, Dk Rosemary aliyezaliwa mwaka 1972, alikuwa mwanamke pekee aliyetia nia kuwania urais kupitia Chadema.

Ana kiwango cha elimu ya Shahada ya Uzamivu ya Maendeleo ya Watu na Shahada ya Uzamili ya Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe aliyoipata mwaka 2006 hadi 2008. Pia amesomea Shahada ya Utawala wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Bangalore nchini India mwaka 1994 hadi 1997.

Kabla ya hapo Dk Majige alisoma stashahada ya masuala ya uongozi katika chuo cha Zeal kilichopo India na masomo ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Tabora mwaka 1997 hadi 1993

Alijiunga Chadema mwaka 2013 akitokea CCM, na miaka saba baadaye, anajipima na kuona kwamba anaweza kumudu kuwania urais kupitia chama hicho.

 

 


Like it? Share with your friends!

-2
-2 points