Vijiji 165 kunufaika na mradi wa maji


1
1 point

Watanzania takribani 500,000 wa vijiji 165 nchini  wanatarajia kunufaikia na huduma bora za maji kutokana na mradi ya kufunga pampu za sola katika maeneo yao.

Taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB), inasema benki hiyo na Serikali ya Tanzania wamesaini mkataba wa msaada wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 4.5 sawa na shilingi bilioni 10.3, kufadhili mradi huo utakaotekelezwa katika mikoa tisa.

Mradi huo wa ufungaji wa pampu zinazotumia nishati ya jua utaondoa utumiaji wa pampu za dizeli ambazo maji yake yamekuwa ni ya gharama na zinachangia uchafuzi wa mazingira kwa kuzalisha gesi ya kaboni.

“Mradi unasaidia kuondoa pengo la uwekezaji katika upatikanaji wa maji vijijini na kuifanya WB kujikita katika kuchangia sekta binafsi kupitia mfuko wa maendeleo wa fedha wa benki ya dunia,” amesema Kaimu Mkuu wa Programu ya GPRBA, Zaruhi Tokhmakhian katika taarifa hiyo.

Katika mradi huo, njia za kidijitali kama ya benki kupitia simu zitatumika ili kudhibiti mapato ya mauzo ya maji, fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya kukarabati miundombinu hiyo.

“Utumiaji wa pampu za sola unatarajia kupunguza gharama za uendeshaji, matengenezo kwa wasambazaji wa maji, kwa kuwapatia wa fedha itasaidia kupunguza bei ya maji na kuongeza mtandao wa huduma, hususani jamii ambazo hazikuwa na huduma,” amesema Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji wa Tanzania, Profesa Kitilia Mkumbo.

Hata hivyo, Mkurugenzi mkazi wa WB, Bella Bird amesema katika mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na maji salama kwa matumizi mradi huo pia utafunga mashine ya kutibu maji (Chlorinators).

“Kupitia mradi huo, tunatangaza teknolojia mpya ya kuiwezesha sekta binafsi kifedha na utoaji wa huduma bora za maji kwa maeneo ya vijijini, ni matumaini yetu kuwa pampu hizo, mita za malipo kabla ya huduma, mashine za kutibu maji na mkataba wa miaka mitano wa matengenezo ni mahususi kwa sekta,” amesema Bird.

 


Like it? Share with your friends!

1
1 point