Uwakilishi wa mawakili watajwa kuwa changamoto nchini


0

Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu Tanzania, Mohamed Chande, amesema pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mawakili nchini wapatao 6,750, bado watu wengi wa mikoani wamekuwa wakikosa uwakilishi wa mawakili wa kujitegemea, huku wengi wao wakitajwa kuzamia mijini pekee.

Amesema makadirio kwa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 58, wakili mmoja anahudumia watu 82,857 wakati Afrika Kusini ambayo inalingana kwa kiasi kikubwa na idadi ya watu, wakili mmoja anahudumia watu 2,500.

Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akitoa mhadhara kuhusu jukumu la wanasheria chipukizi kwa umma na mwelekeo wa sekta ya sheria nchini.

Jaji Chande alisema kuwa wanasheria na mawakili wanatakiwa kwenda kufanya kazi vijijini na kama maofisa wa Mahakama, wakasaidie katika utoaji haki na kuongeza kuwa asilimia 70 ya kesi nchini zipo Mahakama za mwanzo, lakini wananchi wanajiwakilisha wenyewe.

“Katika Mkoa wa Lindi kuna wakili mmoja huku mawakili nane wakiwa katika Mkoa wa Katavi, 20 mkoani Ruvuma, 29 Kigoma na 38 wapo mkoani Mara,” alisema Jaji Chande.

Ameongeza kuwa kuna baadhi ya mikoa takribani saba ya Tanzania Bara haina Mahakama Kuu kama vile Lindi, Katavi, Morogoro, Simiyu, Manyara, Pwani, Singida na Songwe huku wilaya 28 zikiwa hazina Mahakama za wilaya kama vile Mkinga mkoani Tanga.

Jaji Chande alisema ripoti ya dunia ya mwaka 2019 kuhusu utoaji haki inaonyesha watu milioni 230 wanaoishi katika mazingira mbalimbali wanakosa haki, huku watu bilioni 1.5 wanashindwa kutatua matatizo yanayowakabili yanayohusu haki na watu bilioni 4.5 wametengwa na fursa zitolewazo na sheria.

Alisema hali hiyo inaonyesha kutokuwepo kwa usawa au ufikishaji sawa wa haki kwa wote na ukosefu mkubwa wa uwakilishi wa kisheria.


Like it? Share with your friends!

0