Utalii wa Tanzania wafikishwa Korea


0

MWENYEKITI wa Utalii Tanzania (TTB), Jaji Thomas Mihayo na Mkurugenzi Mwendeshaji wa bodi hiyo, Devota Mdachi, wamekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii jijini Seoul, Korea ya Kusini kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania.

Mikutano hiyo, iliandaliwa kwa kushirikiana na ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo, imeanza kufanyika Julai 4 hadi 8, mwaka huu ili kuendeleza mikakati ya kukamata soko la utalii kwa mashariki ya mbali.

Akizungumzia mkutano huo, Jaji Mihayo alisema ziara hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa kutokana na mwitikio mzuri waliopata kutoka kwa wadau wa utalii waliokutana nao.

Alisema ujumbe kutoka TTB, ulifanikiwa kukutana na wadau mbalimbali wakuu wa utalii wa nchi hiyo akiwemo Byeong -Sam Kim ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Utalii wa Korea Ya Kusini (Korean Tourism Assistance).

Katika kikao hicho, TTB na KTA waliweza kufanya mazungumzo yaliyolenga kuhamasisha suala la ushirikiano baina ya mawakala wa utalii wa Tanzania na Korea ya Kusini.

Naye Kim alisema mwaka 2018, idadi ya watalii milioni 26 kutoka Korea Kusini walitembelea nchi mbalimbali duniani.

Aliishauri ili TTB iweze kufanikiwa katika mikakati yake ya kukamata soko la nchi hiyo, ni muhimu kuwaunganisha wafanyabiashara wa utalii wa Tanzania na wenzao wa Korea ya Kusini, alionyesha utayari wake wa kushirikiana na TTB katika kufanikisha suala hilo na aliahidi kwamba ataongoza ujumbe wa mawakala wa utalii kutoka Korea ya Kusini 20 watakaokuja nchini Tanzania katika ziara ya mafunzo itakayofanyika mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Alikubali mwaliko uliotolewa na TTB wa kushiriki katika onesho la kimataifa la utalii la Swahili linaloandaliwa na TTB (S!TE), litakalofanyika Dar es Salaam kuanzia Oktoba 18 hadi 20, mwaka huu.


Like it? Share with your friends!

0