UTAFITI: Asilimia 50 ya Watoto wenye ugonjwa wa figo wamefariki


0

Utafiti uliofanywa na jopo la madaktari bingwa wa figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umebaini asilimia 30 ya watoto wachanga kati ya 380 waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo walipata ugonjwa wa mshtuko wa figo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya figo kwa watoto, Dk. Francis Furia, amesema utafiti huo ulifanyika kati ya mwaka juzi na mwaka jana, ambapo ulibaini kuwa asilimia 50, ya Watoto waliogundulika kuwa na mshtuko wa figo walifariki dunia.

“Kwa sasa kliniki ya figo kwa watoto inayofanyika mara moja kwa wiki, tunawahudumia wagonjwa kati ya 16 hadi 20,” alisema Dk. Furia.

Alisema sababu za kupata magonjwa ya figo kwa watoto ni pamoja na kuugua malaria, dengue, homa ya ini, kuhara, kipindupindu, kupata maambukizi ya bakteria na tatizo la kupumua.

Aliongeza kuwa baadhi ya dawa zinazotumika kutibu magonjwa mbalimbali zimekuwa zikisababisha kupata ugonjwa huo.

“Dawa kama ‘Gentamicin’, ‘Diclofenac’ na ‘Movera’ zimekuwa zikichangia kuongezeka kwa ugonjwa wa figo kwa watoto,” alisema Dk. Furia.

Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni upungufu wa damu, kuvimba uso na tumbo, kiungulia, shinikizo la juu la damu na kushindwa kutoa haja ndogo.

“Wazazi waache tabia ya kuwapa watoto dawa za miti shamba ambazo hazijafanyiwa utafiti, kwani zinaweza kuhatarisha afya ya mtoto na kumsababishia ugonjwa wa figo,” alisema Dk. Furia.

ISHARA KUU ZA UGONJWA WA FIGO

Kwa mujibu wa mtandao wa Kidney Education, dalili za ugonjwa wa figo ni pamoja na kukosa hamu ya chakula, kichefuchefu na kutapika.

Nyingine ni kuwa dhaifu, mwili kuchoka na kupungua uzito, kuvimba miguu, mikono au na usoni karibu na macho pamoja na  shinikizo la damu lisilozuilika, hasa kwa umri mdogo.

Kukosa nguvu kunakosababishwa na upungufu wa damu mwilini (anaemia), hali inayosababishwa na figo kutotengeneza homoni ya erithropoyetini inayosaidia kutengeneza chembechembe za damu.

Kushindwa kulala, kizunguzungu na kushindwa kuwa makini, kujikuna, mkakamao wa misuli, kuhisi uchovu kwenye miguu na kushindwa kufikiria kitu kwa makini.

Kukosa hamu ya kufanya mapenzi kwa wanaume na kukosa hedhi kwa mwanamke  na pia ugonjwa wa figo huhusishwa na ongezeko la vifo vinavyotokana na ugonjwa wa moyo.


Like it? Share with your friends!

0