Usajili waanza upya kwa taasisi zilikumbwa na mabadiliko ya Sheria namba 3


0

Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk Faustine Ndugulile amesema kuanzia leo Jumatano Julai 10, 2019 unaanza usajili wa taasisi zilizosajiliwa kama kampuni lakini zinatekeleza majukumu ya taasisi zisizo za kiserikali (NGO).

Amesema usajili huo umegawanywa katika kanda tano ili kurahisisha mchakato huo.

Dk Ndugulile ametoa kauli leo katika mkutano wa wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ajili ya kuwapa uelewa wa pamoja kuhusu marekebisho ya Sheria namba 3 ya mwaka 2019.

Katika Bunge la bajeti lililomalizika Juni 28, 2019, ulipitishwa muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali kwa mwaka 2019, uliokuwa na marekebisho ya sheria nane, zikiwemo Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali (sura ya 56) na Sheria ya Makampuni (sura ya 212).

Muswada huo ambao umeshapitishwa bungeni mwezi uliopita, unazitaka kila asasi za kirai kujisajili upya,
Dk Ndugulile amesema fomu za maombi ya usajili huo zipo tayari na endapo muombaji akikamilisha taratibu zake kwa ufanisi ndani ya siku 14 atakabidhiwa cheti chake cha usajili ili atekeleze majukumu yake kwa ufanisi.

“Sasa hivi tupo katika kipindi cha miezi miwili ya mpito kuhusu suala hili baada ya Serikali kupitisha sheria. Lakini ikipita miezi miwili tutakuwa wagumu kuongeza muda kwa wale wanaotaka kufanya kazi za NGO lakini hawajajisajili.”

“Tusisubiri dakika za mwisho na sioni sababu za msingi ndani ya siku 60 kwa nini watu wasijisajili kwa sababu tumeweka mfumo wa mchakato huu ikiwemo watu kuomba kwa njia ya mtandano,” amesema Ndugulile.

Amezitaja kanda zitakazotumika kufanya usajili huo ni pamoja na Kanda ya mashariki ambayo kituo chake kitakuwa Dar es Salaam, Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Nyanda za Juu Kusini (Mbeya).


Like it? Share with your friends!

0