Upekee wa hifadhi ya Burigi


0

Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato ambayo imetokana na kuunganishwa kwa mapori ya akiba ya Kimisi, Burigi na Biharamulo ni maarufu nchini kutokana na maliasili za wanyama, mimea na mandhari nzuri ambazo ni kivutio muhimu kwa utalii.

Rais Magufuli, alisema hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,702 na kuifanya ishike nafasi ya tatu kwa ukubwa nchini. Hifadhi inayoshika nafasi ya kwanza ni Ruhaha yenye kilomita za mraba 20,300 ikifuatiwa na Serengeti yenye kilomita za mraba 14,763 iliyoanzishwa mwaka 1959.

Hifadhi nyingine mpya ni Ibanda – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe ambazo zinafanya idadi ya hifadhi zote nchini kufikia 19, mapori ya akiba 23, mapori tengefu 44, hifadhi za misitu 463, misitu asilia 17 na mashamba ya miti 23.

Alisema nchi sasa ina eneo la hifadhi lenye kilomita za mraba 361,594 ambalo ni zaidi ya theluthi moja ya nchi kulinganisha na nchi zingine.

Alitaja baadhi ya nchi na maeneo yao ya hifadhi kwenye mabano kuwa ni Burundi (2,066), Kenya (72,544), Malawi (32,242), Msumbiji (170,662), Rwanda (2,320), Uganda (39,059), Zambia (286,161), Algeria (174,219), Angola (87,507), DRC (324,290), Misri (129,390), Ethiopia (274), Nigeria (127,359) na Afrika Kusini (101,336).

“Ndio maana wakati mwingine huwa tunashangaa watu wanaotutuhumu kwamba hatupendi mazingira, tusingetenga eneo kubwa kiasi hiki au kuanzisha hifadhi tatu kwa mpigo,” alisema Rais Magufuli.

Kuanzishwa kwa Hifadhi za Burigi – Chato, Ibamba – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe kutasaidia kuendeleza na kupanua mtandao wa hifadhi nchini na kuongeza wigo na manufaa ya utalii katika Ukanda wa Kaskazini Magharibi na mapato ya utalii nchini.

Tayari wawekezaji sita wameonyesha nia ya uwekezaji wa kitalii katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato.


Like it? Share with your friends!

0