UNESCO: Idadi ya Watoto wasiokwenda shule yaongezeka


0

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetahadharisha kuwa, kuna uwezekano kwamba, mwaka huu watoto karibu milioni 12 watashindwa kwenda mashuleni kupata elimu.

Taarifa ya UNESCO imesema kuwa, kiwango cha watoto wasiojua kusoma na kuandika hakijabadilika katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi ilioyopita na tathmini mpya zinaonesha kuwa, watoto na barobaro milioni 258 hawakwenda shule katika mwaka uliopita wa 2018.

Taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imesema kuwa, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa watoto wengine milioni 12, hawatakuwa na uwezo wa kwenda shule na kupata elimu mwaka huu.

Imesema katika mazingira ya sasa ni vigumu sana kuweza kutoa elimu bora na ya kiwango kwa watu wote duniani, na kwamba malengo ya ustawi endelevu yaliyoainishwa na jamii ya kimataifa hadi kufikia mwaka 2030 hayatafikiwa.

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa limetahadharisha kuwa, iwapo hakutachukuliwa hatua za haraka za kurekebisha hali hiyo sudusi(1/6) ya watoto wote duniani, itakuwa haijui kusoma na kuandika katika mwaka 2030.

Takwimu hizi za UNESCO zimedhihirisha tena ufa mkubwa uliopo baina ya nchi tajiri na maskini duniani.

 


Like it? Share with your friends!

0