Ubakaji wa mtindo wa Teleza unavyotesa wanawake wa Kigoma


0

Wakati Serikali na Asasi za Kiraia zikipigania kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake, jitihada hizo zinaonekana kuwekewa ugumu kutokana na matukio hayo kuendelea kuibuka huku mengine yakiibuka kwa mtindo tofauti.

Mkoani Kigoma, Wilaya ya Kigoma Ujiji katika Kata ya Mwanga Kusini wanawake wanakabiliwa na ubakwaji na ukatili tangu mwaka 2016, huku nyumba nyingi za wanawake zikivamiwa na wanawake wenyewe wamekuwa katika mateso kufuatia matukio ya ubakaji wa mtindo wa Teleza.

Asasi za Kiraia zipatazo 6 zikiongozwa na Shirika la Twaweza, walifika mkoani Kigoma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuchochea maendeleo ya wananchi katika mkoa huo, lakini baada ya kufika huko wakakutana na visa na mkasa vinavyosababishwa na Teleza, wakajiuliza Teleza ni nani?

Katika uchunguzi wao ikabainika kuwa Teleza ni mtu anaefanya ubakaji akiwa uchi, huku akiwa amejipaka oili chafu au mafuta mengine ili asiweze kukamatwa kiurahisi, pindi anapokamilisha kazi yake ya ubakaji.

Kwa mujibu wa taarifa za Asasi hizo zinaeleza kuwa matukio hayo yanafanana kwa mambo kadhaa ikiwamo, wengi wanaofanyiwa ukatili huo ni wanawake ambao wanaishi bila wanaume ndani ya nyumba zao, Wabakaji huwadhoofisha wanawake wenyewe pamoja na kuwazuia majirani zao au wanakaya, na wengine hutumia dawa za kuwafanya wasinzie au kwa kuwafungia ndani ya vyumba au nyumba zao.

Kadhalika wabakaji hao maarufu kama Teleza, wamekuwa wakitumia silaha hasa visu, mapanga na viwembe ambavyo huvitumia kwa kujihami, kuwatishia na kuwazuia wanawake wasipige kelele.

Inaonekana kwamba wanajamii na viongozi katika eneo hilo hawajalipa uzito suala la wanawake hao na ukatili unaofanywa dhidi yao, waathirika wa mashambulizi hayo mara nyingi hutishwa, huchekwa na kukejeliwa pamoja na kudhalilishwa na Polisi(ambao mara nyingi ni wanaume).

Ripoti ya Asasi hizo za Kiraia zinaeleza kuwa hata wakati wahalifu wanapotajwa na kutolewa ushahidi, ama hakuna hatua zinazochukuliwa, ama wanaume hao hukamatwa kwa muda mfupi kisha kuachiliwa, na wakati mwingine jamii huwashutumu wanawake wanaofanyiwa ubakaji wa Teleza kuwa ni makahaba, na kujenga dhana kwamba kwa namna fulani wanastahili kufanyiwa ukatili huo.

Swala linalowaumiza zaidi wanawake hao wa Kata ya Mwanga Kusini mkoani Kigoma, ambao wanafanyiwa ukatili huo ni kwamba pindi wanapokwenda kupata matibabu hospitalini, wamekuwa wakipata uchungu zaidi kwa kutakiwa kulipa shilingi elfu tano(5000) kwa ajili ya PF3, elfu thelathini(30,000), kwa ajili ya kushonwa na gharama nyingine za matibabu, huku wakiulizwa maswali mengine ya kufedhehesha.

Takwimu kamili juu ya kiwango cha matukio hayo bado hazijapatikana kutokana na changamoto za ukusanyaji wa takwimu kuhusu ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na utayari wa wanawake wengi kusita kutoa taarifa kutokana na hofu ya watu kuwanyanyapaa au wahalifu kulipiza kisasi.

Hata hivyo katika siku tatu za kuchunguza jambo hilo kwa kuwaendea wanawake wenyewe, AZAKI, ziliweza kutambua na kuandika habari za matukio zaidi ya 45 yaliyoanza mwaka 2016 na kuendelea hadi mwaka huu.

Katika kuhakikisha jambo hili linafika ukomo, AZAKI hizo kwa pamoja zimemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ya kumtaka afanye ziara katika eneo la  Wilaya ya Kigoma Ujiji, Kata ya Mwanga Kusini mkoani Kigoma pamoja na kuunda kikosi kazi maalum kitakachojumuisha maafisa wa Polisi, Viongozi wa eneo na wawakilishi kutoka vikundi vya wanawake ili kuchunguza na kushughulikia suala hilo.

 

 


Like it? Share with your friends!

0