TPLB yakata mzizi wa fitina baina ya Kagera Sugar na Stand United


0

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), imebainisha kuwa timu ya Stand United ndiyo itakayoshuka daraja moja kwa moja badala ya Kagera Sugar kama ilivyotangazwa hapo jana kwenye msimamo wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF).

Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura katika mkutano na wanahabari hii leo amewaambia wanahabari kwamba, kulikuwa na makosa katika uingizaji wa matokeo, ya mchezo uliowakutanisha Kagera Sugar na Stand United.

Katika mchezo huo badala ya kuingiza takwimu kuwa Stand wameshinda 3-1, watu wa data kutoka Bodi ya Ligi wakaingiza kimakosa kwa kuandika 3-0, hivyo kuharibu uwiano wa jumla wa magoli ya kufunga na kufungwa baina ya timu hizo.

Aidha kupitia mkutano huo, Wambura amewaomba radhi wadau wa soka kwa kosa lililojitokeza na kusema Ofisi yake inawajibika kwa kumpa adhabu Ofisa aliyepotosha takwimu.

Baada ya takwimu kuwekwa sawa sasa Kagera Sugar itacheza mechi ya play off, Juni 2 dhidi ya Pamba kabla ya kurudiana Juni 8 huku Geita Gold ikicheza na Mwadui katika tarehe hizo.

“Kwanza tuombe radhi kwa mkanganyiko huu uliojitokeza, kulikuwa na kuingiza vibaya kwa takwimu katika mchezo wa Mei 16 kati ya Kagera Sugar dhidi ya Stand ambao wenyeji walifungwa 3-1, lakini watu wetu waliandika 3-0 hapo ndipo kosa lilipoanzia.” alisema Wambura.

 

 


Like it? Share with your friends!

0