Mahakama yatupia mbali kesi ya Zitto Kabwe na wenzake


0

Mahakama nchini Tanzania imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na vyama vya upinzani nchini humo kupinga Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018.

Shauri hilo, lilifunguliwa na muungano wa vyama 10 vya upinzani wakidai unakiuka haki za Kikatiba za kisiasa kwa kuzifanya shughuli mbalimbali za kisiasa kuwa jinai.

Wanasiasa hao wanadai muswada huo unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama hivyo ikiwemo uchaguzi wa viongozi na kusimamisha uanachama kwa wanachama wa vyama hivyo.

Pia walikuwa wanapinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachozuia muswada uliowasilishwa bungeni kupingwa mahakamani.

Hata hivyo, Jaji Benhajj Masoud kayika maamuzi yake leo amekubaliana na upande wa serikali walalamikaji hawakupaswa kuomba Mahakama itamke kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu kinakiuka Katiba na kuomba mahakama itamke kuwa muswada huo unakiuka katiba

Jaji Masoud amesema kwamba shauri hilo linakiuka kifungu cha 8 (2) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu, kwani hawakufuata utaratibu unaoelekezwa katika kifungu hicho.

Kifungu hicho kinaelekeza mtu yeyote anayedai haki zake zinakiuka au zinaelekea kukiukwa anapaswa kutafuta nafuu kwa kutumia njia nyingine zilizopo kwanza kabla ya kwenda mahakamani.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la Tanzania wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo jopo la mawakili wa Serikali, likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo lilidai kuwa walalamikaji hawakukidhi matakwa ya kifungu hicho kwani hawakutumia njia nyinginezo zilizopo kabla ya kukimbilia mahakamani.

Walibainisha kwamba mlalamikaji wa kwanza, Zitto ni mbunge tena mzoefu ambaye anazijua Kanuni za Bunge zikiwemo za mwaka 2016 ambazo zinampa nafasi kushiriki kujadili muswada wowote na kutoa maoni na mapendekezo yake kwa uhuru na zinampa kinga.

Walidai kuwa pia kanuni hizo zinampa mamlaka ya kumuomba Spika aisimamishe kwa muda maalum upitishwaji wa muswaada huo ili kumpa nafasi kuwasilisha maoni yake. Hata hivyo waliiambia mahakama kuwa walalamikaji hawakutumia utaratibu huo kabla ya kwenda mahakamani.

Tatizo liko kwenye nini hasa?

Mlalamikaji wa kwanza Zitto Kabwe baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa watarudi mahakamani kuendelea na shauri hilo.

Tayari mswada huo umeshawasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza mwezi uliopita, lakini je ni mambo gani hasa yanayolalamikiwa kwenye muswada huo?

Kifungu cha 5A kinataka msajili kupewa taarifa kimaandishi na taasisi yeyote ya ndani ama ya nje ya Tanzania itakapotaka kutoa mafunzo ya kiraia ama ya kujenga uwezo kwa chama cha siasa na kutaja wahusika, malengo na nyenzo zitakazotumika katika mafunzo hayo.

Msajili anayo nguvu ya kutoa kibali ama kukataa kufanyika kwa mafunzo hayo na endapo yatafanyika bila kibali taasisi hiyo inaweza kupigwa faini ya mpaka shilingi milioni 30 na watu watakaokutwa na hatia ya kwenda kinyume ni kifungu hicho wanaweza kufungwa kati ya miezi sita mpaka mwaka mmoja gerezani.

Kifungu cha 5B cha muswada kinampa nguvu, msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania kuomba na kupewa taarifa yeyote ile ya chama chochote cha siasa.

Afisaa yeyote wa chama cha siasa ambaye ataenda kinyume na takwa hilo, yaani kutokutoa taarifa husika atakuwa ametenda kosa na akikutwa na hatia atapigwa faini ya kuanzia shilingi milioni moja mpaka kumi au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miezi 12.

Hata baada ya adhabu hiyo, afisaa huyo ama chama hicho bado kitatakiwa kutoa taarifa zilizohitajika na iwapo taarifa itaendelea kumininywa basi chama hicho kinaweza kusimamishwa ama kufutiwa usajili.

Wapinzani Tanzania wanadai iwapo kifungu hicho kitapita, mipango yote ya kimkakati ya vyama vya siasa itakuwa wazi na inaweza kutumiwa na serikali katika kuwaminya.

Hoja yao kuu ni kwamba msajili ni mteule wa rais, ambaye ni mwanachama pia wa chama tawala. Hivyo ofisi ya msajili inaweza kutumika dhidi yao.

Kifungu cha 6 cha muswada kinamlinda msajili na wanyakazi wa ofisi yake dhidi ya kufunguliwa mashtaka: “Shauri lolote halitafunguliwa dhidi ya Msajili, Naibu Msajili, Mkurugenzi ama maafisa wengine chini ya Msajili kwa lolote watakalolifanya ama kutolifanya kwa nia njema chini ya sharia hii,” kinasomeka kifungu hicho.


Like it? Share with your friends!

0