Serikali yakiri uhaba wa wauguzi


0

Serikali imesema itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kadri nafasi zitakavyokuwa zikipatikana ili kuboresha huduma za afya nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema hayo leo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala katika maadhimisho ya Siku ya Waguzi Duniani inayoadhimishwa Mei 12, kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi; Sauti inayoongoza uuguzi kwa dunia yenye afya.”

Waziri Ummy amesema serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kwa sababu kuna uhaba wa wauguzi kwenye vituo vya afya, licha ya kuwapo zaidi ya wauguzi 30,451, katika vituo vya umma na binafsi nchini.

Amesema asilimia 80 ya huduma  za afya katika vituo vya kutoa huduma za afya zinatolewa na wauguzi na kwa hali hiyo, serikali itaendelea kutambua na kuthamini kazi nzuri zinazofanywa na wauguzi nchini.

“Wauguzi wamekuwa wapambanaji wakubwa katika kutoa huduma kwa washukiwa wa ugonjwa wa Covid-19, hivyo hongereni  wauguzi wote nchini Tanzania,” amesema.

Amesema katika jitihada za serikali za kuboresha huduma za wauguzi na wakunga, serikali imekamilisha muongozo wa kutoa huduma kwa kuzingatia utu, heshima na maadili.

Naye Rais wa Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya, amesema ili kuwapo kwa huduma bora na salama za afya, nchi inapaswa kuwa na wataalamu wenye weledi wa hali ya juu na mazingira bora ya kazi.

“Hivi sasa nchi yetu ina wauguzi 30,451 waliojiriwa katika sekta ya afya ambao ni takribani asilimia 60 ya wataalamu wote wa afya. Wauguzi hawa wanatoa zaidi ya asilimia 80 ya huduma za afya ambazo zimekuwa zikitolewa kwa Watanzania. Hivyo upungufu wa wauguzi na wakunga ni  asilimia 48,” amesema Baluhya.

Bw. Baluhya amewapongeza wauguzi  nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona.


Like it? Share with your friends!

0