Sanamu ya Nyerere kugharimu Sh milioni 615


0

Serikali imetangaza kuratibu ujenzi wa sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere kwenye viwanja vya jengo la Amani na Ulinzi la Julius Nyerere lililopo katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia.

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe, ameyasema hayo wakati akisoma hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa idara ya habari (MAELEZO TV), Dk Mwakyembe amesema ujenzi wa sanamu hiyo ni utekelezaji wa azimio la mkutano wa 35 wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Jijini Harare, Zimbabwe mwaka 2015.

 Amesema ujenzi huo utatumia malighafi ya shaba nyeusi na kwamba kamati ya kitaifa ya uratibu na kamati ya ujenzi wa sanamu za kuwaenzi waasisi wa Taifa ziliundwa mwaka juzi kwa mujibu wa sheria ya kuwaenzi waasisi wa Taifa ya mwaka 2004.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi huo, Dk Emmanuel Ishengoma ambaye ni Kaimu Mkurugenzi  wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa katika wizara hiyo amesema, hatua za awali za ujenzi huo zimeanza na mradi unatekelezwa na kampuni ya SAMCRO ya Afrika Kusini, chini ya usimamizi wa SADC na Tanzania.

Amesema ujenzi wa sanamu hiyo unaotarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu, utagharimu takriban Dola 267,992.60 za Marekani (sawa na takriban Shilingi milioni 615 zitakazotolewa na SADC na gharama za usimamizi kutolewa na Tanzania.


Like it? Share with your friends!

0