Samatta atwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika


0

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, jana (Mei 6) usiku amezidi kuidhihirishia dunia ubora wake baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora kutoka Afrika.

Samatta ambaye nyota yake inazidi kung’aa kwa kuendelea kupata mafanikio siku hadi siku akiwa na klabu yake ya Ligi Kuu Ubelgiji, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora, mwenye asili ya Afrika 2019 anayecheza soka nchini Ubelgiji.

Tuzo hiyo hufahamika zaidi kama Ebony Shoe Award, na Samatta anakuwa mchezaji wa tatu wa KRC Genk, kuwahi kutwaa tuzo hiyo baada ya Souleymane Oulare raia wa Guinea ambaye alishinda tuzo hiyo 1999, na Moumouni Dagano raia wa Burkina Faso aliyeshinda tuzo hiyo 2002.

Tuzo hiyo huandaliwa na asasi ya African Culture Promotion, kwa ajili ya kutambua mchango wa wachezaji kutoka Afrika au wenye asili ya Afrika ambao wanafanya vizuri nchini Ubelgiji.

Katika tuzo huyo, Samatta alikuwa akishindana na mshambuliaji Yohan Boli wa Sint-Truiden, kiungo wa Standard Liège, Mehdi Carcela, na Landry Dimata wa Anderlecht.

Mashabiki wengi wa mpira wa miguu hasa kutoka Afrika Mashariki wanatamani kumuona Samatta akiungana na wachezaji wengine wa Afrika kama Victor Wanyama kutoka Kenya, wakikipiga katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Hii inaweza kuwa njia ya yeye kufikia malengo hayo, kwani tayari kuna baadhi ya wachezaji ambao wamewahi kushinda tuzo hiyo na wanacheza EPL, au wamewahi kucheza.

Wachezaji hao ni, Youri Tielemens, Michy Batshuayi, Romelu Lukaku, Marouane Fellaini, Vincent Kompany, Mido, Émile Mpenza na Daniel Amokachi

Samatta ambaye hupenda kutumia kaulimbiu yake ya Haina Kufeli, anaongoza kwa ufungaji wa magoli ya Ligi Kuu Ubelgiji, akiwa ametupia wavuni magoli 23 hadi sasa.


Like it? Share with your friends!

0