Sababu za gharama kuongezeka Hospitali ya Muhimbili zatajwa


0

Wizara ya Afya nchini imesema wagonjwa wanaokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), bila kufuata taratibu za rufaa ndio chanzo cha kuongezeka kwa gharama za vipimo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile bungeni mjini Dodoma leo ambapo amebainisha kuwa  utaratibu wa kupata huduma katika hospitali lazima ufuatwe

Katika swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Kisangi amehoji kwa nini wananchi wanatozwa gharama kubwa mara mbili wanapokwenda kuomba huduma za vipimo.

“Wagonjwa wote ambao wanapitia taratibu za rufaa kuanzia ngazi ya zahanati huwa wanahudumiwa vipimo hivyo kwa gharama ndogo lakini mgonjwa ambaye hajapitia hatua hizo hutozwa gharama kubwa kwani anahesabika kama mgonjwa binafsi,” amesema Dk Ndugulile

Aidha Dk. Ndugulile, ametolea ufafanuzi juu ya changamoto za mashine za kufulia katika hospitali mbalimbali, ikiwemo Mwananyamala, Amana na Temeke, ambapo ameeleza kuwa taratibu za kununua mashine zinaendelea kwani Amana imeshatenga eneo kwa ajili kujenga chumba cha utakatishaji huku wakiwa kwenye mchakato wa kununua mashine kubwa ya shilingi milioni 80.

Amesema Temeke wameshaagiza mashine yenye uwezo wa kufua kilo 70 kwa awamu moja na pasi yake kwa shilingi milioni 83.34 huku Mwananyamala ikiwa imeagiziwa  mashine mbili za shilingi milioni 71 na tayari moja imeshapelekwa katika Hospitali hiyo.

 


Like it? Share with your friends!

0