Profesa Kabudi asisisitiza demokrasia


0

Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi ameeleza mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali nchini katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya ya madola, ikiwa ni pamoja na suala la demokrasia na tawala bora.

Mambo mengine yaliyoelezwa na Profesa Kabudi katika mkutano huo ni masuala ya usalama, biashara, namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira.

Taarifa iliyotolewa jana na wizara hiyo kuhusu mkutano huo unaofanyika nchini Uingereza imeeleza kuwa Profesa Kabudi alieleza hayo katika majadiliano ya taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyokubaliwa katika mkutano wa marais na wakuu wa Serikali wa nchi wanachama wa umoja huo ulifanyika mwaka 2018 nchini humo.

Kabudi aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa Tanzania imeendelea kutekeleza maazimio ya mkutano uliopita kwa kusimamia ipasavyo misingi ya demokrasia na utawala bora na haki za binadamu.

“Na pia imehakikisha kuwa inatoa huduma bora za kijamii kwa watu wote ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, na pia imeongeza bajeti na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kujenga hospitali na vituo vya afya, nyumba za watumishi wa afya na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba,” alisema Profesa Kabudi.

Waziri huyo alisema Serikali inaendelea kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama na pia kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini na mijini ili kuchochea maendeleo katika maeneo yote ya nchi.

Aidha ameongeza kuwa katika kutekeleza maazimio ya Umoja huo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na uchafuzi wa mazingira, Tanzania tayari imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia tarehe Juni Mosi mwaka huu na amewahakikishia wajumbe kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa chanya.

Katika ufunguzi wa mkutano huo, katibu mkuu wa jumuiya ya madola, Patricia Scotland alisema jumuiya hiyo inafanya mageuzi ya kiutawala ili iweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi miongoni mwa nchi wanachama.


Like it? Share with your friends!

0