Polisi wanne kortini kwa mauaji ya Mmarekani mweusi


0

Minnesota, Marekani

Polisi wa jimbo la Minnesota, Derek Chauvin (44) aliyesababisha kifo cha Mmarekani mweusi, George Floyd, sasa atashtakiwa kwa mauaji badala ya mashtaka ya awali ya mauaji ya kutokukusudia.

Chauvin anadaiwa kumkandamiza Floyd kwa goti na kumsababishia kifo hicho, huku maafisa wengine watatu, Tou Thao, Thomas Lane na Alexander Kueng waliokuwepo katika eneo la tukio wakishtakiwa kwa kusaidia na kushawishi mauaji hayo.

Mwanasheria Mkuu jimboni humo, Keith Ellison, amesema hatua hiyo imefikiwa ili kupata haki ya Floyd, familia yake, jamii na serikali.

Mashtaka hayo yamefanyika ikiwa ni zaidi ya juma moja tangu Floyd kuuawa akiwa chini ya ulinzi wa polisi, hali iliyoamsha maandamano nchi nzima yakipinga ukatili wa polisi dhidi ya weusi nchini Marekani.

Chauvin, alikamatwa juma lililopita na dhamana yake imeongezeka hadi dola millioni 1 mpaka kufikia jana jumatano. Maafisa wengine watatu wamewekwa chini ya ulinzi wa polisi jana na wanashikiliwa kwa dhamana ya dola million 1.

 

 

 


Like it? Share with your friends!

0