Polisi Marekani walikoroga tena


0

MAREKANI

Nchini Marekani katika mji wa Buffalo uliopo New York, Polisi wawili wameonekana wakimshambulia mzee mwenye umri unaokadiriwa kuwa miaka 75 ambaye hakufahamika mara moja.

Tukio hilo limeshutumiwa na watu wengi hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa polisi hao walisimamishwa kazi bila malipo jana Alhamisi, baada ya video hiyo kuonekana.

Tukio hilo limetokea wakati bado Wamarekani wakiwa katika maandamano ya amani dhidi ya kifo cha George Floyd yanayoendelea kwa takribani siku ya kumi.

Video ya ukatili huo mpya ilirekodiwa na mwandishi wa habari kutoka kituo cha redio cha umma cha WBFO, na kuchapishwa kwenye wavuti yake na akaunti ya twitter inaonyesha mtu huyo mzee mwenye nywele nyeupe anakaribia safu ya maafisa wa polisi .

Polisi mmoja alionekana anamsukuma kwa kutumia moja ya vifaa vinavyotumika kuzuia ghasia, na wa pili akatumia mkono wake kufanya vivyo hivyo.
Sauti ilisikika baada ya mzee huyo kuanguka chini, kisha damu ilianza kutiririka kutoka kwenye kichwa chake.

Meya wa Buffalo, Byron Brown amesema katika taarifa yake kuwa, baada ya siku za maandamano ya amani na mikutano kadhaa kati yake na polisi na wanajeshi, tukio la kusukumwa mzee huyo limekuwa baya kwake.

Kwa mujibu wa Meya Brown, Kamishna wa Polisi huko Buffalo, ameagiza uchunguzi kufanyika na kuwasimamisha kazi polisi hao wawili.

Naye Gavana wa New York, Andrew Cuomo ameandika kwenye akaunti yake ya twitter kwamba, alizungumza na Meya Brown na kukubali kwamba maafisa waliohusika wanapaswa kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Andrew Aliandika katika mtandao wake wa Tweeter “Maafisa wa Polisi lazima watekeleze sheria na sio kuitumia vibaya sheria.”


Like it? Share with your friends!

0