Polisi Marekani kama sikio la kufa…


-1
-1 points

MAREKANI

Mauaji ya Mmarekani mweusi mwingine Rayshard Brooks (27) aliyepigwa risasi na polisi katika mji wa Atlanta – Georgia Ijumaa jioni, yamesababisha shutuma mpya kwa polisi dhidi ya utumiaji wa nguvu kupita kiasi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza (BBC), Meya wa Atlanta, Keisha Lance Bottoms amethibisha kuwa Mkuu wa Polisi wa mji huo, Erika Shields, amejiuzulu juzi Jumamosi kufuatia kitendo hicho.

Maandamano mapya yalizuka katika siku za mapumziko ya mwishoni mwa juma, wakishinikiza hatua zaidi zichukuliwe kufuatia kifo cha Brooks.

Katika picha za video zilizosambaa zinaonesha Brooks akikataa kukamatwa baada ya kufanyiwa vipimo vya kubaini hali yake au ikiwa ametumia mihadarati; na kuanza kupambana na polisi wawili hadi akafanikiwa kuwachomoka.

Lakini afisa mwingine wa polisi alitumia silaha ya umeme kumnasa Brooks, kisha polisi hao wawili walitoweka kwenye video hiyo huku milio ya risasi ikisikika na baadaye, Brooks alionekana akiwa amelala chini karibu na mgahawa wa Wendy’s.

Idara ya uchunguzi ya Georgia inachunguza kifo hicho na inatafuta video za kamera za usalama ndani ya mgahawa wa Wendy’s na picha za mashuhuda.

 

Kisa hicho kimejiri ikiwa ni wiki chache zimepita baada ya mauaji ya Mmarekani mweusi George Flody kutokea na kuzua maandamano makubwa ulimwenguni.


Like it? Share with your friends!

-1
-1 points