Nyungu ya mwarobaini haina madhara


0

TANZANIA

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya, amesema mti wa mwarobaini hauna madhara yeyote kwa watumiaji, bali una manufaa kwa tiba asili ya magonjwa mbalimbali.

Profesa Mgaya amesema, kumekuwepo taarifa zisizo sahihi zilizochapishwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii, zikimnukuu kusema mti huo ni miongoni mwa ambayo haifai kujifukiza kwa sababu una kemikali zenye sumu, jambo ambalo si kweli.

“Mti wa mwarobaini unatibu magonjwa arobaini, majani yake yanatumika kutibu minyoo, magamba yanatumika kutibu homa na mafuta ya mti huo yanatumika kutengeneza sabuni kwa ajili ya ngozi, hivyo mti huu ni mzuri na una manufaa makubwa kwa jamii yetu,” amesema Profesa Mgaya.

Ameongeza kuwa, NIMR ilifanya utafiti na kupata njia mbili za kumpa nafuu mtu mwenye maradhi mbalimbali ambazo ni dawa lishe na kujifukiza kwa kutumia mimea au majani ya miti tofauti inayosadia kufunguka kwa mishipa ya damu, kifua kinachobana na kuondoa uchovu na msongo wa mawazo.

Kituo hiki kilinukuu taarifa ya awali na kuchukua kwa uzito taarifa hii ya Profesa Mgaya. hivyo tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.

Tunauhakikishia umma kwamba tutaendelea kuchapisha taarifa sahihi zisizochuja, zikiwemo za elimu na hamasa ya kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Kwa umoja wetu, tutaitokomeza corona Tanzania.

 


Like it? Share with your friends!

0