Ndugai: Kuna umuhimu wa kuwapa wachezaji wetu lishe nzuri


0

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema miongoni mwa sababu iliyochangia Stars kupoteza mchezo wa kwanza jana dhidi ya Senegal ni lishe duni ya wachezaji wetu.

Spika Ndugai ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam akitokea Misri aliposhuhudia mchezo wa kwanza wa Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Senegal na Tanzania uliomalizika kwa Taifa Stars kuchapwa 2-0.

Ndugai alisema wachezaji wa timu pinzani (Senegal) walikuwa na miili mizuri ambayo inatokana na lishe nzuri.

“Kuna umuhimu wa kuwapa wachezaji wetu lishe nzuri ya kutosha ili kushindana na wapinzani wa aina ya Senegal,” alisema Ndugai.

Katika hatua nyingine Ndugai aliwageukia viongozi soka na michezo mingine nchini akisema wengi siyo watu sahihi wa kuongoza sekta hiyo ya michezo.

Ndugai aliungana na wabunge wengine kwenda Misri kuwapa morali wachezaji na makocha wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) alisema Watanzania tumeachia michezo kama ni vile mtu yoyote anaweza kuongoza kitu ambacho siyo sahihi vivyo kuna ulazima wa kuanza mchakato kupata viongozi wazuri katika michezo.

“Wakipatikana viongozi wazuri wataweza kuongoza klabu zetu mbalimbali mpaka vijijini huko, wilayani na mikoani,” alisema.

“Tunatakiwa kuondoa rushwa katika michezo ili kupiga hatua kwani ni miongoni mwa sehemu inayoturudisha nyuma katika michezo mingi na kushindwa kufanya vizuri,” alisema Ndugai.


Like it? Share with your friends!

0