Ndugai ataka kanuni za usafri wa majini zipitiwe


0

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameitaka Serikali kupitia upya kanuni za usafiri wa majini kwa ajili ya kuangalia viwango vya mizigo wanavyotozwa.

Spika Ndugai ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akiunga mkono swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Mariam Msabaha, ambapo amesema kiwango cha mzigo wa kilo 20 kutozwa fedha ni kidogo sana kwani hata begi la mwanafunzi linazidi uzito huo, huku akihoji hata mashirika ya ndege yanatoza kilo zaidi ya hizo.

Awali Msabaha ameuliza ni mzigo kiasi gani ambao abiria anapaswa kulipia ushuru wa bandari kwani mzigo wa kilo 20 wasafiri wa kwenda Zanzibar wanatozwa shilingi 9,750.

Msabaha pia ameomba Serikali kueleza ni lini matamko yanayotolewa ndani ya Bunge yatafanyiwa kazi kwa uhalisia, kwani hali ni mbaya kwa boti za Bakhresa kila wakati kukiuka masharti.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa amesema mizigo inayotakiwa kutozwa ni yenye uzito wa kilo zaidi ya 21. Kwandikwa amesema abiria wanaotumia bandari kwenda Zanzibar kwa boti kwenye eneo “Baggage room”, ni wale tu wanaokuwa na mizigo mikubwa tena kwa madhumuni ya kibiashara.

Kuhusu boti za Bakhresa amesema wataliangalia jambo hilo kutokana na malalamiko kuwa mengi kwa abiria wanaotumia usafiri huo.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wateja wanaotumia bandari kwenda Zanzibar kwa boti wapime mizigo yao kabla ya kupakia ili wajue uzito wake  kama wanastahiki kutozwa ushuru wa bandari.


Like it? Share with your friends!

0