Mugabe atazikwa wapi?


0

Familia ya rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe, na serikali ya nchi hiyo, wameendelea kutofautiana kuhusu ni wapi Mugabe anapaswa kuzikwa.

Hata tarehe kamili ya kuzikwa kwake bado haijulikani, baada ya familia kupinga mpango wa serikali, kwamba apewe mazishi ya kitaifa katika makaburi ya mashujaa mjini Harare. Familia ya Mugabe imesema wanataka azikwe kijijini kwao Kutama. Mkutano kati ya Rais Emmerson Mnangagwa na mjane wa Mugabe Bi. Grace Mugabe kusuluhisha tofauti hizo, umefeli kupata suluhisho.

Mwili wa Mugabe uliletwa Zimbabwe siku ya Jumatano kutoka Singapore, alikofariki akipokea matibabu.

Hapo jana watu kadhaa walijeruhiwa mjini Harare Zimbabwe, kufuatia mkanyagano uliotokea kwenye uwanja, wakati waombolezaji waliopiga foleni, waliposukumana wakitaka kuutizama mwili wa rais huyo aliyeiongoza Zimbabwe kwa miaka 37.

Msemaji wa serikali ya Zimbabwe amesema viongozi 10 wa Afrika, wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya kiongozi huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 95.

Miongoni mwa viongozi hao wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya Mugabe ni pamoja na Rais wa Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa, Uhuru Kenyata, Kenya, Rais wa China Xi Jinping na kiongozi wa zamani wa CUBA Raul Castro.


Like it? Share with your friends!

0