Sikupotea, nilitekwa na kutekwa kwangu kumetokana na masuala ya kisiasa? – Mdude ?


0

Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mdude Nyagali amesema hakupotea kama ambavyo taarifa zilivyoripotiwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Mimi nilitekwa wala sikupotea, lile eneo mimi nimeishi kwa miaka 20, siwezi kupotea hata kama nitatembea nikiwa nimefungwa macho” Alisema Mdude 

Katika mazungumzo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hii leo, Mdude ameuthibitishia umma kuwa tukio la kutekwa kwake limetokana na sababu za kisiasa kwa kuwa amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Rais Dk. Magufuli.

Ninathibitisha kuwa tukio lililonitokea ni la kisiasa sio la kijambazi maana maisha yangu ni chini ya dola 100 kwa mwezi, sasa jambazi gani atakuja kuniteka mimi” Alihoji Mdude Nyagali

Aidha, Mdude Nyagali amesema tukio la kutekwa kwake linahusishwa na siasa kwa ushahidi kwamba waliomteka waling’ang’ania nyaraka za chama chake na hata maneno waliyokuwa wakizungumza watekaji yalitosha kuthibitisha kuwa tukio lake ni la kisiasa.

“Kama siyo tukio la kisiasa kwanini waniambie niite Umoja wa Mataifa waje wanisaidie, kwanini waliniambia nimwambie Mbowe na Lissu waje wanisaidie?” Alihoji Mdude

Awali akitoa simulizi ya kutekwa kwake, Mdude Nyagali alisema kuwa watu watatu ambao walijitambulisha kuwa ni askari polisi walimfuata na kumwambia anatuhumiwa kwa kumtukana Rais na Serikali yake kupitia mitandao ya kijamii hivyo wamekuja kumchukua kwa mahojiano zaidi.

Polisi waliwahi kukanusha kuhusika na taarifa za kutoweka kwa Mdude na kwa mujibu taarifa waliyoitoa ni kwamba wanafanyia uchunguzi tukio la kutoweka kwake. Hii siyo mara ya kwanza kwa Kada huyo wa Chadema kutekwa na kuteswa kwani mwaka 2016, Mdude aliwahi kutekwa na kuteswa kisha kufunguliwa kesi ambayo baadae alishinda kesi hiyo. 


Like it? Share with your friends!

0