MC Pilipili afikishwa mahakamani


-1
-1 points

Mshereheshaji Emmanuel Mathias (34), maarufu kama MC Pilipili na mwenzake, Heriel Clemence (25), wamefikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kuchapisha maudhui kwenye mtandao bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka  ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Costastine Kakula, akisaidiana na Batrida Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.

Kakula alidai washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhui bila kuwa na leseni. MC Pilipili ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach na Clemence Mkazi wa Kawe, wanatuhumiwa kutenda makosa hayo kati ya Novemba 17, 2013 na Mei 2, 2019 katika maeneo tofauti tofauti ndani ya jijii la Dar es Salaam, kupitia televisheni ya mtandaoni inayojulikana kama Pilipili TV .

Washtakiwa hao walikana kuhusika na tuhuma hizo, ambapo Kakula alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambore, aliomba Mahakama itoe masharti nafuu ya dhamana kwa wateja wake, kwa sababu shtaka linalowakabili linadhaminika.

Hakimu Mmbando alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana, kila mmoja anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua halali za utambulisho na vitambulisho halali ambao watasaini bondi ya shilingi milioni tano kwa kila mmoja.

Hata hivyo, MC Pilipili alikamilisha masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana, ambapo Clemence alishindwa kukamilisha kutokana na nyaraka za wadhamini wake kutokamilika, lakini leo inatarajiwa kesi hiyo kuja tena kwa ajili ya kukamilisha masharti, na itasubiriwa hadi Juni 4


Like it? Share with your friends!

-1
-1 points