Mbunge apigia debe matumizi ya bangi


0

Wakati Serikali hapa nchini ikipinga matumizi ya bangi, huku wanakamatwa nayo wakiishia mikononi mwa dola, Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM) ameishauri Serikali iruhusu matumizi ya bangi kwa kile alichodai kuwa mmea huo unatumika kutengenezea  dawa nyingi za maumivu.

Kishimba ametoa pendekezo hilo wakati akichangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, kwa mwaka wa fedha 2018-2019, ambapo ameiomba wizara hiyo, kuchukua hatua za makusudi ili kuweza kuruhusu mmea huo ulimwe na wakulima hapa nchini.

“Sisi wenyewe tunayo bangi ukweli bangi hiyo sio kwa ajili ya kuvuta ni inaenda ,Lethoto na Zimbabwe wameruhusu. Gunia moja la bangi ni milioni 4 mpaka 5, bangi yote hii ya Tanzania inaenda katika madawa ya binadamu kuna ubaya gani Serikali itoe vibali ili watu walime bangi? Waziri wa Kilimo awasiliane na wa Afya kwani bangi hailiwi na wadudu ekari moja ya bangi unapata gunia sita” amesema Kishimba.

Hoja ya Kishimba imeonekana kumfurahisha Spika Job Ndugai, ambaye aliwaomba wabunge wengine kuchangia kama ambavyo amechangia mbunge huyo, kwa kujikita sehemu moja.

“Niwape siri muongee kama Kishimba unakuja na kitu chako fulani.unajikita sehemu moja.Hii hoja ni nzito sana, naamini Jenista (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge, Ajira, Kazi, na watu wenye ulemavu) ameipigia mstari,” amesema Spika Ndugai.

Hata hivyo hoja ya aina kama hiyo zimewahi kutolewa na wabunge wengi hapa nchini lakini bado kama Serikali imeendelea kuweka msimamo wake kutokana na kwamba matumizi ya bangi yamekuwa yakiwaathiri zaidi vijana.


Like it? Share with your friends!

0