Marekani yazidi kutoa tahadhari ya corona Tanzania


0

TANZANIA

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tena tahadhari kwa raia wake waliopo nchini kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya COVID 19 kufuatia hatua ya serikali ya Tanzania kutotangaza hali ya maambukizi ya virusi vya corona tangu April 29 mwaka huu.
Katika taarifa yao waliyoitoa kwenye tovuti, inasema kuwa ubalozi upo tayari kutoa Pasi za kusafiria za dharula kwa raia wake waliopo nchini wanaotaka kurudi Marekani.
Taarifa inasema licha ya Tanzania kufungua sekta ya biashara na shughuli za kijamii, hatari ya kupata maambukizi ya COVID 19 kupitia jamii inayowazunguka ni kubwa.
Ubalozi huo unasema vituo vya afya vinaweza kuzidiwa katika kutoa huduma, Uwezo mdogo wa hospitali za Tanzania unaweza kutishia maisha kwa kuchelewa kupata huduma za dharula.

Ubalozi napendekeza wafanyakazi wake waliopo nchini pamoja na familia zao kuendelea kuchukua tahadhari katika shughuli zao za kila siku ikiwemo kudhibiti wageni wanaowatembelea majumbani na kuvaa barakoa wanapotoka nje ya nyumba zao, kuosha mikono mara kwa mara na kuepuka misongamano.
Wamewataka Raia wake waliopo Tanzania wanaohitaji kuondoka kuangalia ratiba za ndege za kimataifa kwenye mtandao kwani serikali ya Tanzania imeruhusu baadhi ya ndege za abiria za kimataifa kufanya safari zake.

Hii si tahadhari ya kwanza kwa ubalozi wa Marekani nchini kuitoa kwa raia wake kuhusu COVID 19, ya kwanza ilitoka Mei 25 ikafuatiwa na ya June 2 na June 11 zote zikisistiza kuwa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona ipo juu jijini Dar es Salaam.


Like it? Share with your friends!

0