Marekani Yazidi ‘kukomalia’ Corona Tanzania


-5
-5 points

Dar es Salaam, Tanzania

Ubalozi wa Marekani nchini umetoa tahadhari mpya ya afya kwa kusisitiza kuwa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona bado ipo juu katika jiji la Dar es Salaam.

Tahadhari hiyo iliyotolewa Jumanne jioni na kuchapishwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya ubalozi huo, inawaonya raia wa nchi hiyo waliopo nchini hususani Dar es Salaam, kuendelea kuchukua tahadhari.

Pia tahadhari hiyo imeeleza kuwa takwimu mpya za ugonjwa wa corona ikiwemo vifo hazijatolewa nchini Tanzania tangu Aprili, 29 mwaka huu.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni wiki moja tangu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kumhoji Kaimu Balozi wa Marekani, Imni Peterson kuhusu tahadhari zilizotolewa hapo awali.

Baadaye, taarifa ya serikali ilitolewa ikieleza kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo Wilbert Ibuge amesikitishwa na namna ubalozi huo umekuwa ukitoa tahadhari zake.

Moja ya masuala yaliyolalamikiwa na serikali ni pamoja na madai ya ubalozi huo kuwa hospitali nyingi za Dar es Salaam zimefurika wagonjwa wa COVID-19, jambo ambalo serikali inasema si kweli.

Hivi karibuni, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Elisha Osati aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa mfumo wa afya nchini haujaelemewa na corona kama inavyoelezwa.

Jumatatu wiki hii, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema idadi ya wagonjwa wa COVID – 19 ambao bado wamelazwa hospitalini ni wanne kwa Tanzania Bara.

 

 


Like it? Share with your friends!

-5
-5 points