Marekani yakamata meli ya Korea


0

Serikali ya Marekani imetangaza kukamata meli ambayo ni mali ya Korea Kaskazini, na kuilaumu kwa kukiuka vikwazo vya kimataifa dhidi ya taifa hilo ambalo limekuwa kwenye mgogoro kutokana na mpango wake wa kurutubisha silaha za nyuklia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Haki ya Marekani, meli hiyo ilitumika kusafirisha makaa ya mawe ambayo ndiyo biashara kubwa ya taifa hilo licha ya kupigwa marufuku na Umoja wa Mataifa, kuendelea kuyauza nje ya mipaka yake.

Aidha, imeelezwa kuwa meli hiyo imewahi kukamatwa nchini Indonesia Aprili mwaka 2018.

Hii ni mara ya kwanza Marekani kuikamata meli ya Korea Kaskazini kwa kukiuka vikwazo, na hatua hiyo inajiri wakati ambapo uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umedorora kupindukia.

Mkutano kati ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na rais wa Marekani, Donald Trump, uliisha bila makubaliano Februari mwaka huu, huku Marekani ikiisisitizia Korea Kaskazini kusitisha mpango wake wa kinyuklia huku naye Kim Jong Un alisisitiza kuondolewa vikwazo.

Korea Kaskazini imetekeleza majaribio mawili ya makombora yake angani katika kipindi cha wiki moja, katika kile kinachoonekana kuwa jaribio la kuishinikiza Marekani kufanya makubaliano.

Meli hiyo kwa jina The Wise Honest, ilikamatwa mara ya kwanza mwaka uliopita na Marekani ilitoa kibali cha kuikamata Julai 2018. Indonesia imeikabidhi Marekani meli hiyo na sasa inaelekea Marekani.


Like it? Share with your friends!

0