Mapato yaongezeka sekta ya madini


0

Hatua za Serikali kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao na kuongeza mapato zimeanza kuzaa matunda, licha ya kupingwa vikali hapo awali.

Akiongea na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amesema hatua zilizochukuliwa kwenye sekta ya madini  na kuboresha mifumo ya kukusanya mapato ya Serikali imechangia kuongeza mapato maradufu.

Akieleza hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Dkt. Abbasi amesema ni pamoja na ujenzi wa ukuta kwenye eneo la migodi ya madini ya Tanzanite Mererani, kuanzishwa kwa masoko ya madini kwenye mikoa na wilaya nchi nzima na kuundwa kwa mifumo ya kisasa ya kijiditali ya kurekodi mapato ambayo licha ya kuongeza mapato, lakini pia imeongeza ufanisi.

Aidha amesema kuwa hadi kufikia mwezi Mei 2019, sekta ya madini kwa kipindi cha miezi kumi na moja ya mwaka wa fedha 2018/19, mapato yamefikia Shilingi bilioni 302.63 kiasi ambacho ni zaidi ya mapato yote, kiasi cha Shilingi bilioni 301.6 yaliyopatikana kwenye mwaka wa fedha 2017/18.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Dkt. Abbasi mapato kwenye sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne yamekuwa yakiongezeka mfululizo, akitolea mfano amesema mwaka 2016/17 makusanyo ya maduhuli yalikuwa bilioni 214.5, wakati mwaka 2015/16 maduhuli yalikuwa Shilingi Bilioni 210 na mapatao ya mwaka 2017/18 yalikuwa Shilingi bilioni 301.6.

Aidha, aliongeza kuwa mapato yanayotokana na mauzo ya madini ya Tanzanite tangu ujenzi wa ukuta wa Mirerani ujengwe kuzunguka migodi ya madini hayo, mapato yameongezeka maradufu kutoka kiasi cha shilingi milioni 71.8 mwaka 2015 hadi kufikia bilioni 1.43 mwaka 2017.


Like it? Share with your friends!

0