Mama Maria Nyerere augua ghafla


0

Mke wa baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amelazwa katika Hospitali jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili nchini jana Jumatano Juni 5, 2019, akitokea Kampala Uganda alipokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, limeandika kuwa mtoto wake Makongoro Nyerere amesema, baada ya kuwasili nchini mama yake alipumzishwa kwa muda wakati madaktari wakiendelea na uchunguzi kabla ya kufikia uamuzi wa kumlaza.

Makongoro alisema alipelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam, akitokea Kampala nchini Uganda alikokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.

Mama Maria Nyerere alikwenda Uganda, Namugongo kwa ajili ya kuhiji. “Sukari ya Mama ilipanda ghafla na kulazimika kupelekwa hospitali ambako baada ya uchunguzi madaktari walimruhusu asafiri kuja Dar es Salaam baada ya afya yake kuimarika kidogo,” alisema Makongoro.

Hija hiyo ambayo miaka yote Rais Yoweri Museven wa Uganda huwa anashiriki, mwaka huu aliahirisha muda mfupi na kwenda kumjulia hali Mama Maria hospitalini Uganda alikokuwa amelazwa.

Inaelezwa kuwa Mama Maria amekuwa akisafiri kutoka Tanzania kwenda Namugongo kwa miaka 13 mfululizo, kushiriki sherehe hizo za hija ambazo hujumuisha waumini wa Kikristo kutoka nchi mbalimbali.


Like it? Share with your friends!

0