Mali za Mugabe kupigwa Mnada leo


0

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe, anapiga mnada mali zake kadhaa ikiwemo matrekta makubwa na ya kisasa matano na zana nyengine za kilimo.

Tangazo lililotolewa na kampuni ya kunadisha mali, linaonesha kuwa Mugabe amepanga kuuza magari yapatayo 40, ikiwemo gari moja la kifahari na magari matano aina ya Toyota Hilux pick-up.

Wachambuzi wanaamini hatua hiyo ya kuuza mali inaweza kuashiria kuwa biashara ya familia ya Mugabe ambayo inamiliki mashamba makubwa 21 inaweza ikawa inapitia wakati mgumu wa kifedha.

Mnada huo unatarajiwa kufanyika leo Jumamosi, na kuongozwa na kampuni ya Ruby Auctions katika shamba lake la Gushungo.

Shamba hilo lipo katika eneo maarufu na la kifahari, na ndani yake kuna jumba la makazi la kifahari pia.

Familia ya Mugabe ilijimilikisha shamba hilo wakati wa utekelezwaji wa sera ya kupora mashamba, yaliyokuwa yakimilikiwa na walowezi wa kizungu nchini Zimbabwe.

Mwaka 2015, mke wa Mugabe, Bi Grace Mugabe aliwafukuza kwa kutumia nguvu wanakijiji ambao waliingia na kuweka makazi ndani ya shamba hilo.

Gazeti la Herald la nchini Zimbabwe, limeripoti kuwa bado haijulikani sababu ya mnada huo lakini limedai kuwa biashara ya familia hiyo iliyojengwa katika miaka 37 ya Mugabe madarakani, inapitia kipindi kigumu kwa kushtakiwa mara kwa mara kwa kushindwa kulipa madeni.

Mugabe, ambaye ana miaka 95, alipelekwa nchini Singapore kwa matibabu mwezi uliopita, na atarajiwa kurejea nyumbani katikati ya mwezi huu, shirika la habari la kimataifa la AFP limemnukuu raisi wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa akisema.

 


Like it? Share with your friends!

0