Malecela asema na vijana wa CCM


0

Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela amewataka vijana kuendeleza mipango iliyofanywa na wazee katika kukilinda Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuhakikisha kinaendelea kuwa imara.

Malecela ameyasema hayo leo Jumatano Julai 10, 2019 wakati akitoa salamu kwenye kikao cha ndani cha viongozi wa chama na serikali ambacho kiliitishwa mahususi kwa ajili ya kumsikiliza Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Katika kikao hicho kilichofanyika Ndungu, Same Mashariki, Malecela amesema wao ambao kwa sasa ni wazee, walipambana na kuweka mipango iliyosababisha CCM kuwa imara hadi sasa na kwamba kwa sasa ni kazi ya vijana kuendeleza mpango huo.

“Sisi tuliofikia hapa, tuliweka mpango na kukisimamia chama na hadi sasa kiko imara, sasa vijana muendeleze mpango ili CCM iendelee kuwa imara,” amesema Malecela

Aidha amewataka pia viongozi kuanzia ngazi ya mashina hadi wilaya kusimama imara na kushirikiana kuhakikisha CCM inashinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka 2019 na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya amesema chama kimeendelea kuimarika na kuwa na mvuto kwa wananchi hatua ambayo inatoa ishara ya chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2020.


Like it? Share with your friends!

0