Malecela amfariji Moremi wa maabara ya Taifa


0

Aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela, amemfariji Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, Dk Nyambura Moremi, huku akimtabiria kupata mafanikio makubwa siku chache zijazo.

Moremi na Meneja wa Udhibiti wa Ubora wa maabara hiyo, Jacob Lusekelo, wamesimamishwa kazi Mei 4, mwaka huu, hatua iliyochukuliwa siku moja baada ya Rais John Magufuli kutilia shaka utendaji wa upimaji wa virusi vya homa kali ya mapafu (COVID-19) katika maabara hiyo.

Agizo la kusimishwa kazi kwa wawili hao, lilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwa kumuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kwa utekelezaji.

Akihutubia mjini Chato wakati akimuapisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba, Rais Magufuli alisema hivi karibuni zilitumwa sampuli zisizo za binadamu kwenye maabara hiyo kwa siri, na kurudisha baadhi ya majibu yakionyesha uwepo wa COVID-19 kwa wanyama, ndege na matunda.

Kupitia ukurasa wake wa twitter, Dk Malecela ameandika “ Nyambura Moremi, haijalishi unajisikiaje kwa sasa, elewa hivi…hili jambo pia litapita.  Utaruka na kuitazama siku hii  kwa tabasamu kwa sababu itakufanya kuwa mkubwa na mtu bora. Inaweza isifikirike hivyo kwa sasa lakini niamini, siku njema kwako zipo mbele yako. Ishi kwa amani!”

Malecela aliondolewa kwenye wadhifa wa NIMR usiku wa kuamkia Disemba 17, 2016 baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake pasipo kutajwa sababu.

Lakini hatua hiyo ikahusishwa na taarifa ya kuwepo ugonjwa wa Zika nchini zilizotolewa na Dk Malecela, na baadaye kukanushwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.


Like it? Share with your friends!

0