Magufuli atoboa siri ya wakwepa kodi


0

Rais wa Tanzania Dk.John Magufuli, amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitengeneza vitabu vya hesabu ili kukwepa kupeleka kodi kubwa ya ongezeko ya thamani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Magufuli ameyasema hayo leo katika mkutano kati yake na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini unaojadili changamoto wanazokutana nazo na kuzitafutia majibu.

Amesema linapofika suala la kuwasilisha asilimia 18 ya VAT, wengi wamekuwa wakibaki nayo kama mtaji badala ya kuipeleka serikalini huku akibainisha wamekuwa wakitengeneza vitabu tofauti.

“Kimoja ni cha benki chenye mahesabu ya kweli yenye faida na kitabu kingine ni cha TRA. Kwa kawaida kile kinachopelekwa benki kinakuwa cha kweli lakini kinachoenda TRA ni kidogo wakati mwingine kinaonyesha hasara,” amesema

Ameongeza kuwa “Nataka nitoe mfano wa kampuni tatu, moja ya kampuni (Jina linahifadhiwa) ina vitabu vitatu na fedha zake ni hatari ukiangalia, nina uhakika huyo mfanyabiashara ataenda akairudishe hiyo hela iliyokuwa inatakiwa,” amesema

“Kampuni nyingine namba mbili (Jina linahifadhiwa) taarifa ya benki inaoyesha mwaka 2017 inaonyesha faida ilikuwa shilingi milioni 958 , lakini iliyopelekwa TRA ni shilingi milioni 20 kwenye kitabu cha pili, kampuni namba tatu mwaka 2017 taarifa ya benki inaoyesha faida ilikuwa shilingi milioni 501 lakini TRA iliambiwa kuwa imepata faida ya Sh72 milioni.”

“Kampuni hiyohiyo mwaka 2018 ilipeleka benki shilingi milioni 508, huku kitabu cha TRA kikionyesha ni shilingi milioni 3. Kampuni namba nne ilipeleka kitabu benki chenye taarifa ya faida ya shilingi bilioni 5.03 lakini TRA waliambiwa kuwa wamepata faida ya shilingi milioni 255.”

Majina ya kampuni hizo tumezihifadhi kwani hazijapatikana kuelezea kwa kina madai hayo.

Pamoja na hayo Rais Magufuli amekiri kwa kusema Serikali bado haijawawekea mifumo mizuri kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, kitu ambacho kimekuwa kikifanya biashara nyingi kuzorota hapa nchini.


Like it? Share with your friends!

0