Maandamano ya George Floyd yafika Ikulu


1
1 point

Washington, Marekani

Jimbo la Washington nchi Marekani limetangaza amri ya kutotoka nje ili kukabiliana na ghasia zilizosababishwa na kifo cha Mmarekani mweusi aliyekamatwa na polisi.
Maandamano yamefika karibu na Ikulu (White House) hali iliyosababisha Usalama wa Taifa kumpeleka Rais Donald Trump kwenye chumba cha chini cha ardhi ambacho kilitumika wakati wa mashambulio ya kigaidi zamani
Mabomu ya machozi yametumika kutawanya waandamanaji zaidi ya 1,000 waliokuwa nje ya Ikulu hiyo na mabango huku wakiimba na kuwasha moto.

Takribani watu 4,100 wamekamatwa kutokana na makosa ya kuvunja maduka, kufunga barabara na kutozingatia muda wa kutotoka ndani.
Zuio la kutokutoka nje limewekwa Washington pamoja na miji mingine ikiwemo Atlanta, Chicago, Denver, Los Angeles, San Francisco na Seattle lengo ni kudhibiti waandamanaji wanaopinga ukatili unaofanywa na Polisi
Lakini amri hiyo imepuuzwa katika maeneo mengi huku bidhaa madukani zikiibiwa, magari yakichomwa moto na majengo yakiharibiwa.

 

Rais Trump ametoa wito wa utulivu kufuatia kifo cha George Floyd na amesema hataruhusu magenge ya wahalifu kutumia kifo hicho kutekeleza vitendo vya uhalifu.
George Floyd alifariki dunia Jumatatu iliyopita katika mji wa Minneapolis baada ya afisa wa polisi Derek Chauvin kumkandamiza shingoni kwa kutumia goti.

Maafisa wote wa polisi waliokuwepo kwenye tukio hilo wamefukuzwa kazi na Afisa Chauvin tayari ameshitakiwa kwa mauaji ya Floyd,
Chauvin alionekana katika kanda ya video akipiga goti kwenye shingo la Floyd kwa dakika kadhaa huku Floyd akisikika akisema kuwa hawezi kupumua.

 


Like it? Share with your friends!

1
1 point