Lissu abwagwa kesi ya kupinga ubunge


0

Mahakama Kuu imekataa maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma.

Mahakama imesema mwanasheria mkuu huyo wa Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Katika viunga vya Mahakama hii leo wafuasi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, walifurika huku wengi wao wakiwa na matumaini ya ushindi wa shauri hilo lakini mambo yakenda tofauti.

Akisoma uamuzi huo wa Mahakama leo Jumatatu Septemba 9, 2019 Jaji Sirillius Matupa, amesema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Lissu alifungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kumwakilisha, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake na Mahakama itengue  taarifa hiyo.

Nje ya Mahakama Freeman Mbowe, amesema pamoja na uamuzi wa Mahakama, lakini bado wana Imani na muhimili huo katika kutafuta haki, hivyo wataendelea kuutumia kwani safari ya kutafuta haki ni ndefu huku akinukuu baadhi ya maneno ya marehemu Nelson Mandela.

“Tunasafari ndefu sana katika kutafuta haki, hata Rais Nelson Mandela ameandika hayo katika kitabu chake cha Long walk to freedom. Niseme jambo moja sisi kama chama tunaimani na muhimili huu hivyo tutaendelea kuufuata ili tupate haki zetu”- Freeman Mbowe

Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku akijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko, na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


Like it? Share with your friends!

0