Kwaheri Pierre Nkurunziza


-1
-1 points

BURUNDI

Maelfu ya raia wa Burundi wamejitokeza leo kumuaga aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, hayati Pierre Nkurunziza yaliyofanyika katika Mji Mkuu wa Gitega uliopo katikati mwa Burundi.

Rais wa sasa, Jenerali Evariste Ndayishimiye ameongoza mazishi ya Nkurunziza aliyefariki dunia Juni 8 mwaka huu kwa mshtuko wa moyo.

Wananchi wamejitokeza pembezoni mwa barabara ambapo msafara wa mazishi umepita kuanzia katika hospitali iliyopo mkoa wa Karusi, ulipohifadhiwa mwili wake hadi Gitega huku kukiwa na ulinzi wa hali ya juu.

Leo imetajwa kuwa siku ya mapumziko nchini humo ili kupisha mazishi na watu wote waliohudhuria waliombwa kuvaa nguo nyeupe.

Nkurunziza alifariki ikiwa imesalia miezi miwili kabla ya kukabidhi madaraka kwa mrithi wake, Rais Ndayishimiye aliyeshinda kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Mei, mwaka huu.

Nkurunziza aliiongoza Burundi kwa miaka 15 tangu mwaka 2005, alipochaguliwa mpaka 2020 alipoachia madaraka.

Kabla ya kujiunga na masuala ya siasa mwaka 1995, Nkurunziza alikuwa mwalimu wa mazoezi ya viungo katika moja ya shule za sekondari nchini humo.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi ndio ilimwingiza Nkurunziza katika siasa kwani alikuwa sehemu ya wapiganaji wa kilichokuwa kikundi cha waasisi cha CNDD-FDD.

Baada ya vita hivyo, CNDD–FDD ilibadilika kuwa chama cha siasa na Nkurunziza akawa kiongozi wa chama hicho mwaka 2000, na baadaye aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais Agosti 2005.

Mwaka 2015, aligombea tena na alichaguliwa kwa muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi uliokuwa na utata.

Lakini Juni, 2018 Nkurunziza alisema hatogombea tena baada ya muhula wake wa sasa kumalizika mwaka 2020.

Hatimaye Mei mwaka huu Burundi ilifanya uchaguzi na mgombea urais kupitia CNDD-FDD, Evariste Ndayishimiye alishinda.

Nkurunziza atakumbukwa kwa masuala kadhaa yaliyoleta utata katika uongozi wake ikiwemo kitendo cha kubadilisha muhula wa urais kutoka miaka mitano kuwa saba, hatua ambayo ingemruhusu kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.

Pumzika kwa amani Pierre Nkurunziza.

 

 


Like it? Share with your friends!

-1
-1 points