Kiza kinene kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda


0

Katibu mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga amewataka waandishi wa habari kutonyamazia tukio la kutekwa kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani, Azory Gwanda.

Azory alitoweka Novemba 21, 2017 katika mazingira ya kutatanisha kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana, ambapo mpaka sasa hajapatikana.

Mukajanga ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC).

“Azory si mtu pekee aliyepotea na hilo halitufanyi sisi kama wanataaluma wenzake tuone hicho kitu ni sahihi na tufumbie macho, alipotea katika eneo lenye tatizo,” amesema Mukajanga.

Amesema kuna hisia kuwa kupotea kwa Azory kunatokana na kazi yake, maana aliripoti mauaji na kupotea kwa watu wengine katika eneo lake la kazi.

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo MCT, imeandaa malalamiko kwa ajili ya kukusanya saini kutoka kwa wadau mbalimbali na kuzipeleka Wizara ya Mambo ya ndani, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na kwa mkuu wa mabalozi nchini.

Amebainisha kuwa licha ya malalamiko hayo kuandaliwa zaidi ya miezi mitano sasa, mwitikio umekuwa mdogo kwa maelezo kuwa wiki mbili zilizopita saini 288 pekee ndio zilikuwa zimekusanywa.

“Tunamuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ahakikishe uchunguzi unafanywa kuhusu kupotea kwa Azory na katika malalamiko hayo tunaomba Serikali itamke kwamba Azory amepotea,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko amesema, yanapotokea matatizo ya waandishi wa habari haipaswi kuachiwa mtu mmoja, au taasisi fulani isipokuwa yanatakiwa kushughulikiwa na kila mmoja kwa nafasi yake.

End


Like it? Share with your friends!

0